Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akitoa pole kwa mke wa hayati Benjamini Mkapa Mama Anna Mkapa nyumbani kwake Msaki Jijini Dar es Salaam. |
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametia saini
kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin
William Mkapa kilichotokea jijini Dar es Salaam na ametoa pole kwa familia kwa
niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali.
“Ndugu wanafamilia, kwa niaba ya Mheshimiwa
Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali tumepokea taarifa za msiba wa mzee
wetu, kiongozi wetu Rais wa Awamu ya Tatu kwa masikitiko makubwa. Nawasihi
muendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kama
alivyosema Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai
24, 2020) nyumbani kwa marehemu Masaki, jijini Dar es Salaam. Amewasihi
wanafamilia na Watanzania kwa ujumla waendelee kumuombea marehemu kwa
Mwenyezi Mungu kwa sababu yote ni mapenzi yake.
Amesema kamati ya mazishi ya Serikali
inaendelea na maandalizi pamoja na kuwasiliana na viongozi kutoka katika nchi
marafiki ambao marehemu alifanya nao kazi ili kutoa fursa ya wao kushiriki.
“Tutatoa taarifa ya ratiba ya kuaga mwili itakayofanyika Uwanja wa Taifa.”
Kufuatia kifo hicho kilichotokea usiku wa
kuamkia leo, Rais Dkt. Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya Kitaifa
kuanzia leo Ijumaa, Julai 24, 2020 na katika kipindi chote cha maombolezo
bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Akitangaza kifo hicho kwa Watanzania kupitia
vyombo vya habari usiku wa kuamkia leo Rais Dkt. Magufuli kwa masikitiko
makubwa alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini William Mkapa amefariki
dunia hospitalini jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Rais Dkt. Magufuli amewataka Watanzania wote
wawe watulivu na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na
mpendwa wao Mhe. Benjamin William Mkapa. “Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba
mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu
amefariki dunia.”
Aliongeza kuwa “ Amefariki dunia katika
hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania
tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais
Mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye ametangulia mbele za haki.”
0 Comments