POLISI KIGOMA YAPIGA MARUFUKU WAGANGA WA JADI MAARUFU "KAMCHAPE"

Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Jeshi la polisi Mkoani Kigoma limepiga marufuku watu wanaosadikiwa kuwa waganga wa jadi maarufu kwa jina la "Kamchape" na "lambalamba" ambao wamekuwa wakizunguka katika vijiji mbalimbali wakidai kufichua wachawi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma kamishna msaidizi wa polisi Filemon Makungu akiwahutubia mamia ya wananchi katika kijiji Cha Mkongoro wilayani Kigoma amesema shughuli zinazofanywa na watu hao ni haramu na ni kinyume cha sheria za nchi.

"Nataka kuwaambia, hao watu ni matapeli ,wachonganishi, hawana vibali vya kufanya wanayofanya, hivyo tutaendelea kuwakamata wao pamoja na wanaowaita, nawaomba mzingatie heria" amesema Kamanda Makungu.

Aidha Kamanda Makungu amesema kazi hiyo ya kufichua wachawi imeleta uhasama mkubwa katika familia na jamii kutokana na dhana inayoanza kujengeka sasa kuwa kila mtu anayekufa au kuugua anakuwa amerogwa hali ambayo inasababisha wananchi wengi kuishi kwa hofu.

Amesema Jeshi la polisi kwa kushirikiana na idara nyingine za Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya hali hiyo ili kuhakikisha wananchi wanaelewa madhara huku ikichukua hatua kali kwa wanaoendesha shughuli hizo.

Kwa upande wao wananchi wamepata nafasi ya kumuuliza Kamanda wa polisi maswali na kutoa maoni juu ya watu hao, ambapo wameliomba Jeshi la polisi kutowaingilia kwa kuwa hatua hiyo inatokana na wao kuchoshwa na matukio ya kichawi katika maeneo yao.

John Joseph mkazi wa Mkongoro amesema, wanachofanya Kamchape si cha kumuonea mtu bali ni kuwabaini wachawi na kuteketeza zana zao na kwamba hatua hiyo imesaidia kupunguza vitendo vya kishirikina.

Post a Comment

0 Comments