WAAJIRI MKOANI KIGOMA WATAKIWA KUTONYANYASA WATUMISHI







Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka waajiri katika  Sekta za Umma na binafsi mkoani Kigoma kuacha tabia ya kunyanyasa watumishi bali kuzingatia  miongozo ya kazi zao ili  kulinda haki na stahiki za watumishi hao

Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza na wafanyakazi wa Mkoa wa Kigoma kwenye  kilele cha maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Mji  Kasulu. 

Amesema ni vizuri Menejimenti za Taasisi kuweka utaratibu wa kukutana na viongozi wa vyama huru vya wafanyakazi ili   kuvifanya vyama hivyo kuwa daraja  baina ya waajiri na waajiriwa. 

Amefafanua kuwa, Vyama vya wafanyakazi visibebe jukumu la kusimamia maslahi ya watumishi pekee bali vijikite pia katika kutoa Elimu ya Kanuni na Sheria kwa watumishi sambamba na kujenga utaratibu wa kukutana mara kwa mara na pande zote mbili yaani waajiri na waajiriwa ili kutatua changamoto zao. 

"Mitazamo ya kujikita upande mmoja imekuwa ikichangia sana kukuza migogoro baina ya watumishi na waajiri wao hali inayosababisha kuzorota kwa  upatikanaji wa matokeo chanya katika utendaji kazi hali inayosababisha kukosekana kwa huduma bora kwa wananchi"  amesema Andengenye. 

Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa mkoa amewataka watendaji hao kuwa mabalozi kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuihamasisha jamii kushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. 

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi mkoani Kigoma Jumanne Hamis ameiomba Serikali kushauriana na taasisi za kibenki ili ziweze kupunguza riba kwenye mikopo ya wafanyakazi. 

Aidha Katibu huyo ameiomba Serikali kurejesha kikokotoo cha awali katika utoaji wa malipo kwa wastaafu sambamba na kuwataka waajiri kuzingatia miongozo ya serikali katika kulipa kima cha chini cha mshahara kwa watumishi kuendana na kanuni na taratibu za serikali. 

Katika hatua nyingine katibu huyo wa TUCTA amempongeza Rais Dkt.. Samia Suluhu kwa kupandisha madaraja ya mishahara kwa watumishi wa Umma pamoja na kushughulikia maslahi ya watumishi walioondolewa kazini kutokana na changamoto za vyeti vya kitaaluma.

Post a Comment

0 Comments