Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizungumza na Meneja wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Kanda ya Arusha Ndg Idd Mkomalasa wakati alipotembelea kukagua bidhaa zinazozalishwa na Bodi hiyo akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Arusha hivi karibuni. |
Muonekano wa vihenge vya kuhifadhia nafaka vya
Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Jijini Arusha pamoja na baadhi ya ofisi
zikiwa katika uchakavu
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
WAZIRI wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa siku 14 kwa Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko Dkt Anslem Moshi kukamilisha
malipo ya wakulima wote waliouza korosho msimu wa mwaka 2018/2019.
Waziri Hasunga ametoa agizo hilo wakati alipotembelea na kukagua
shughuli za utendaji kazi zinazofanywa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko
Jijini Arusha.
Amesema kuwa Bodi hiyo ilipewa dhamana la kununua korosho mwaka
2018 kwa niaba ya serikali na tayari serikali imeshatoa fedha zote kwa ajili ya
wakulima lakini bado CPB haijakamilisha malipo hivyo ni lazima malipo
yakamilike ndani ya siku hizo.
“Ndani ya siku 14 sitaki kusikia malalamiko ya wakulima lazima
wakulima wote wawe wamelipwa fedha zao haraka iwezekanavyo” Alisisitiza
Katika ziara hiyo pia Waziri Hasunga amemuagiza Mkurugenzi Mkuu
wa Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko kuwasilisha haraka mpango kazi wa namna
viwanda hivyo vitakavyofanya kazi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa
zitakazohitajika na wateja na kukidhi matarajio ya serikali ikiwa ni pamoja na
kuainisha idadi ya watumishi wanaohitajika.
Hasunga ameiagiza kampuni ya Monaban ambayo ilikuwa imekodisha
kiwanda hicho kutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa mwaka jana ya
kuhamisha mali zao zote zilizopo katika eneo hilo la serikali kwani kesi
mahakamani na notisi ilishaisha.
Akiwa kiwandani hapo Waziri Hasunga amebaini uchakavu wa mitambo
iliyopo pamoja na uchache wa watumishi wanaofanya kazi katika kiwanda hicho
hivyo ameagiza kufanyika ukarabati wa majengo hayo kuanzia mwezi Agosti badala
ya Octoba kwa taasisi hiyo ilivyopanga.
“Tukisubiri mpaka mwezi wa kumi tutakuwa tumechelewa kwa kuwa
mvua zitaanza kunyesha jambo ambalo litapelekea kushindikana kufanyika
ukarabati” Amesema
Amesema kuwa Lengo la serikali ni kufufua viwanda kwa ajili ya
kuongeza thamani ya mazao ya nafaka nchini ili kuzalisha bidhaa mbalimbali kama
unga N,k na kuuza katika masoko ya ushindani ndani na nje ya nchi.
0 Comments