WAZIRI WA KILIMO: HAYATI MZEE MKAPA ALISISITIZA ELIMU YA KILIMO KWA WALIKULIMA TANZANIA

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akikagua mazao mbalimbali ya mizizi wakati alipotembelea Jijini Arusha kufungua maonesho ya kilimo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI SERIAN Jijini Arusha.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye maonesho ya kilimo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI SERIAN Jijini Arusha

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akikagua shamba la maharage wakati alipotembelea Jijini Arusha kufungua maonesho ya kilimo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI SERIAN Jijini Arusha



RAIS wa awamu ya tatu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamini Mkapa wakati wa utawala wake aliainisha kuwa
 nia na lengo kuu la sekta ya kilimo ni pamoja na kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanapata elimu na ujuzi wa kutosha wa vitendo, hivyo Wizara ya Kilimo inatakiwa kujizatiti kikamilifu kuwasaidia wakulima kuishi katika uchumi wa viwanda.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alibainisha hayo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye maonesho ya kilimo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI SERIAN Jijini Arusha na kuongeza kuwa Mkapa alieleza dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa inafikia uchumi wa kati na wa viwanda kwa kuwa na uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo.

“Hayati Rais Mkapa wakati wa utawala wake alilisisitiza kuwa nchi yoyote ili iwe na Usalama na Amani ni lazima wananchi wawe wamejitosheleza kwa chakula endapo kutakuwa na upungufu wa chakula ni dhahiri kuwa nchi haiwezi kuwa na utulivu wa kisiasa na kimaendeleo’’ Alisema

Pia Hayati Mkapa alipiga vita kwa nguvu kubwa umasikini ambapo alianzisha kauli mbiu ya MTAJI WA MASIKINI NI NGUVU ZAKE MWENYEWE ikilenga kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuchagiza shughuli za maendeleo.

Kadhalika Hayati Benjamin Mkapa alisisitiza ulazima wa maafisa Ugani kufanya kazi mashambani kwa wakulima badala ya kuishi mjini pekee kwani kwa kufanya hivyo watawasaidia wananchi kunufaika na kilimo kwa kuwa na tija kubwa katika uzalishaji hivyo kuwa na kilimo cha kibiashara.

Waziri Hasunga alisema kuwa Hayati Rais Mkapa alikuwa muumini wa teknolojia bora za kilimo hivyo aliitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa inatumia teknolojia na zana bora za kilimo ili kuhakikisha kuwa malighafi zinazotokana na mazao ya kilimo zinaendelea kuzalishwa kwa wingi.

Kadhalika, Hayati Mkapa alisema kuwa kilimo bila utaalamu hakiwezi kumkomboa mkulima hivyo aliagiza Taasisi za utafiti wa Kilimo na vyuo vya mafunzo ya ufundi kuhakikisha kuwa vinaendeleza juhudi za kuimarisha elimu kwa wananchi na wakulima ili kuwa na taifa bora lenye wakulima wazuri.

 

 



Post a Comment

0 Comments