SERIKALI KUTUMIA NGUVU KUDHIBITI WAKIMBIZI KIGOMA

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene akizungumza na wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene akicheza ngoma ya Kirundi sambamba na wacheza ngoma hiyo ambao pia ni wakimbizi.

Na Mwandishi Wetu, Kasulu Kigoma

SERIKALI imesema itatumia nguvu kubwa katika kudhibiti raia wa Burundi wanaoingia nchini na baadaye kuingia katika maeneo ya msitu wa hifadhi wa Makere Kusini na Kaskazini uliopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kufanya uharibifu mkubwa na kufanya kilimo cha bangi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene, alisema hayo  wakati wa ziara yake mkoani Kigoma wakati akizungumza na wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu, ambapo pia alieleza hatua mpya zitakazoanza kuchukuliwa kwa wakimbizi wasiokuwa na vibali vya kuwa nchini.

“Kuanzia sasa utaratibu uliokuwa unatumika wa kuwarejesha wale waliokuwa wanakamatwa bila vibali wakiwa wametoroka kwenye makambi hautafanyika tena ila tutafanya mchakato wa kisheria wa kuwa tunawapeleka gerezani, utaratibu wa kutopelekwa magerezani nimeufuta kuanzia sasa tutawapeleka huko, hatuwezi kuvumilia hali hiyo” alisisitiza Waziri Simbachawene.

Wakati huo huo Waziri Simbachawene alisisitiza kuwa Tanzania haitatoa tena uraia kwa wakimbizi kutoka Burundi na kuwataka warejee nchini kwao huku Balozi mdogo wa ubalozi wa Burundi mkoani Kigoma Kabura Cyriaque, akiwataka warundi warudi nyumbani na kwamba serikali yao ni serikali mzazi wa kila raia wa Burundi.

“Kile kilichotokea cha kutoa uraia wa jumla kwa idadi kubwa  hakitatokea tena kwasababu hata wale ambao walipewa uraia wamebakia makambini hawajaenda kuchanganyikana huko kwenye jamii, kila mtu akitoka hapa wazo lake liwe ni kurudi nyumbani” alisema Waziri Simbachawene.

“Kama tulivyowaambia serikali iliyoko madarakani kwasasa ni serikali mzani nan i serikali inayofanya kazi” alisema Barozi Mdogo wa Burundi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange, alimueleza Waziri Simbachawene kuwa maeneo mengi ya Wilaya ya Kasulu, yamejaa wahamiaji haramu ambao baadhi yao huingia katika msitu wa hifadhi ya Makere wakijifanya wanalima kumbe huficha silaha ambazo huzitumia kufanya uhalifu.

“Kwa uchunguzi wetu katika kijiji cha Kitanga ambapo ndio tunapakana na Burundi ndio sehemu ambayo siraha nyingi zinaingia kutoka Burundi, yani watu wanaotoka Burundi wakiingia Tanzania wanabadirishana Sub machine gun na gunia moja la mahindi au la maharage” alisema Kanal Anange

Post a Comment

0 Comments