WATOTO WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU WASAIDIA VITANDA NA MAGODORO

 

Bi.Mwanayasha Hamis akiwa amebeba wanae mapacha wakifurahia zawadi ya godoro na kitanda walichokabidhiwa na waumini wa Kanisa la African Inland Mkoa wa Kigoma.kama sehemu  ya huduma ya idara ya huduma ya mama na mtoto kwa kanisa hilo. (Picha na Magreth Magosso Kigoma) 


Waumini wa Kanisa la African Inland Mkoa wa Kigoma(AICT).wakiongozwa na Askofu  Silasi Kezakubi (mwenye koti rangi ya kahawia) wa Dayosisi ya Tabora wakiomba baraka za Mungu juu ya zawadi ya magodoro 15 na vitanda 15 kabla ya kukabidiwa wahusika.(Picha na Magreth Magosso, Kigoma )


Na Magreth Magosso, Kigoma 

WAUMINI wa Kanisa la African Inland (AICT) Mkoa wa Kigoma wamefanikiwa kuwapa na kuwaongezea faraja watoto 15 waishio katika mazingira magumu baada ya kuwakabidhi vitanda na magodoro.

 

Zawadi hizo zimekabidhiwa jana baada ya ibada ya kubariki watoto katika kanisa hilo ukiwa ni mpango wa kutimiza ndoto za  watoto waishio katika mazingira magumu na kuwezeshwa usingizi mororo kupitia kitanda na godoro zuri kwa usalama wa afya zao.

 

Akifafanua hilo Mratibu wa Kituo cha huduma ya mama na mtoto AICT Kigoma Robart Chamungu alisema kituo kina watoto 247 lakini magodoro 15 na vitanda 15 ni kwa ajili ya watoto wenye uhitaji wa vifaa hivyo.

 

"Tunalea watoto wenye mazingira magumu kwa lengo la kupunguza changamoto zinazowakabili katika  familia wanazoishi na kati ya watoto 247, watoto 15 tu watanufaika na msaada huu huku wengine wakinufaika na vyakula vya msingi ambapo kila mwisho wa mwezi wanapewa mahitaji yao ya  msingi."alisema Mratibu wa kituo hicho.

 

Alieleza kuwa kupitia mpango  wa mwaka wa fedha wa 2020/21 kwa mashirikiano na washirika wenza   Asasi ya Compassion yenye makao yake mkoani Arusha wataendelea kupunguza changamoto za watoto waliosajiliwa katika kituo hicho kulingana na bajeti yao.

 

Alisema huduma  zingine wanazotoa kwa watoto wa kituo hicho ni pamoja na elimu ya roho na elimu ya dunia sanjari na matibabu ikiwa ni mkakati wa kuwafariji watoto wenye mazingira magumu.

 

Akikabidhi vifaa hivyo Askofu Silasi Kezakubi wa Dayosisi ya Tabora aliwasihi waumini wa madhehebu hayo wamtumikie mungu kwa ajili ya kanisa na watu wenye uhitaji.

 

"Nipo katika ziara ya mkoa wa Kigoma na kesho Katavi  lengo  kuzungumza na wakristo, kuokoka ni kujitoa kwa kutoa zawadi kwa wengine. Hakuna mtu asiyeweza kusaidia mwingine, wanaotoa wengi ni watu wenye maisha ya kawaida” alisema

 

Aidha ameikumbusha jamii isimamie misingi ya malezi ya watoto wote bila kubagua, kitendo cha kumnyoshea kidole mtoto wa mwenzako kwa tabia mbovu sio suluhisho badala yake umkanye kwa kumuelimisha athari ya vitendo viovu kwake na jamii kwa ujumla. 

 

Hata hivyo KGPC Blog imezungumza na Mwanayasha Hamisi ni miongoni mwa wanufaika 15 wa zawadi hizo, alisema hana cha kuwalipa zaidi ya kuwakabidhi mikononi mwa Mungu wazidi kubarikiwa na kazi za mikono yao.

 

Naye Rebeka Mihuri ni mmoja wa wanufaika wa huduma ya Mama na Mtoto alikuwa na haya “nasaidiwa na Kanisa la African Inland Mkoa wa Kigoma kwa malazi, chakula, elimu, matibabu ya afya hatimaye leo napewa godoro kwa kuwa kitanda tulikuwa nacho nyumbani, nawashukuru”.

 

Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments