CCM KUPELEKA UMEME KISIWA CHA GANA

 


CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kupeleka umeme kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza.


Hayo yalisemwa jana (Ijumaa, Septemba 25, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa, Kassim Majaliwa katika mkutano wa kampeni katika kitongoji cha Gana. Katika mkutano huo, Mheshimiwa Majaliwa alimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea mbunge, Bw. Joseph Mkundi na madiwani wa wilaya hiyo.


Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ijayo kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025, itaboresha huduma ya umeme katika visiwa vyote nchini kikiwemo Gana chenye wakazi zaidi ya 3000. "Mkakati wetu ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata umeme, Ukerewe vijiji 70 tayari vina umeme vimebaki sita ambavyo vitapitiwa na mradi," alisema Majaliwa.


Alisema asilimia 80 ya vijiji nchini vimepata umeme baada ya Serikali ya awamu ya tano kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020. “Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuendeleza na kuimarisha sekta ya nishati ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali. Mpango wa Serikali ni kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote na maeneo ya pembezoni mwa miji.”

 

Akizungumzia kuhusu ununuzi wa kivuko katika kisiwa hicho, Majaliwa alisema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutoa kivuko kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo Kata ya Ilangala, wilayani Ukerewe.

 

Alisema Ilani ya CCM imetoa maelekezo kwa Serikali ijayo itekeleze idadi kubwa ya miradi ya kimkakati ikiwemo kuboresha usafiri wa majini ili kuwandolea adha wananchi wanaoishi katika maeneo ya visiwani.


Majaliwa alisema wananchi zaidi ya 3000 wa Gana, wanahitaji kivuko bora ambacho kitatoa fursa kwao kufanya shughuli za uvuvi na biashara ili kujipatia kipato.


"Hapa Gana tutaleta kivuko, hiki kisiwa ni kikubwa kina idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma bora ya usafiri wa majini. Serikali yenu imeweka mipango mizuri kwa ajili yenu," alisema Mheshimiwa Majaliwa.

 

Post a Comment

0 Comments