CCM KUTOWAVUMILIA WANACHAMA NDUMILAKUWILI

 Na Mwajabu Hoza, Kigoma

CHAMA cha Mapinduzi CCM kimeeleza kutokuwa tayari kuwavumilia wanachama wa chama hicho ambao wana tabia ya  ndumila kuwili mchana wamevaa mavazi ya CCM  usiku wanakaa kwenye vikao kukiponda chama.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa chama hicho Amandus Nzamba wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho wilaya ya Kasulu Mji ambapo amesema chama hakitaki watu wenye tabia hizo katika kipindi hiki cha uchaguzi.

“Wale ambao mchana CCM jioni vyama vingine safari hii tutawashughulikieni wale ndumila kuwili ambao saa hizi wamevaa kijani lakini usiku mko kwenye vikao sasa vijana wetu watakuwa nyuma yenu hatutaki aibu katika mkoa wetu” alisema  Nzamba

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kigoma Amandus Nzamb akizungumza na wananchi wilaya ya Kasulu Mji wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho wilayani humo.(Picha Zote na Mwajabu Hoza)

Wakati huo huo katibu wa chama hicho Kajoro Vyohoroka amesema katika kipindi cha miaka mitano ambayo wananchi walikiamini chama na kukipatia jukumu la kuongoza, mambo mengi ya maendeleo yamefanyika ikiwemo miundombinu ya barabara, reli, elimu, afya maji lakini pia kuifikisha nchi katika uchumi wa kati.

Kajoro amesema hayo yote yametokana na chama kuwa imara katika kusimamia utekelezaji wa ilani yake ambayo imekuwa ikitekelezwa vizuri na serikali hivyo kuomba wananchi kutoa ridhaa kwa mara nyingine ili mambo mengi mazuri yaendelee kutekelezwa kupitia ilani ya CCM.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Kigoma Kajoro Vyohoroka akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kasulu Mji wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama hicho wilayani humo.

Aidha katika uzinduzi huo mgombea ubunge wa jimbo la Kasulu Mji kupitia chama hicho Prof. Joyce Ndalichako amesema licha ya kufanya mengi katika sekta ya elimu ndani ya wilaya hiyo bado ana deni kubwa kwa wakazi wa Kasulu na kuahidi kulitimiza pindi wakimpa nafasi ya kuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Ndalichako amesema wananchi wa Kasulu wanakabiliwa na adha kubwa ya miundombinu ya barabara za mitaani ambazo zinahitaji matengenezo lakini pia huduma bora ya maji safi na salama kwa wananchi wa jimbo hilo bado ni changamoto kwa baadhi ya maeneo na hivyo kuahidi kuwa mambo hayo yatakuwa kipaumbele kwake.

“Serikali ya chama cha mapinduzi imedhamiria kuendelea kuondoa kero ya maji sehemu ambazo zina uhaba wa maji, sasa mimi kama mpambanaji mwenye mahusiano mema na watu na hili likiwa ni dhamira ya chama nitashirikiana na serikali kuhakikisha wanaanza utekelezaji katika wilaya ya Kasulu”.

Mgombea ubunge jimbo la Kasulu Mji kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Prof Joyce Ndalichako wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Ndalichako amezindua kampeni zake huku akisindikizwa na baadhi ya wagombea ubunge wa Mkoa wa Kigoma akiwemo Dkt. Philipo Mpango mgombea ubunge jimbo la Manyovu pamoja na Atashasta Nditiye jimbo la Muhambwe ambao wamesema ndani ya kipindi cha miaka mitano amejitahidi kupandisha kiwango cha elimu kwa watoto wa Kitanzania kupata elimu iliyobora na isiyo na mashaka yoyote hivyo ni vyema kumpatia nafasi ili aweze kufanya mambo mengi mazuri katika wilaya ya Kasulu.
Wananchi wilayani Kasulu Mji wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho wilayani Kasulu mkoani Kigoma.




Post a Comment

0 Comments