Na Mwajabu Hoza, Kigoma
KATIBU mkuu wizara ya
viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe amemtaka mwekezaji wa kiwanda
cha chumvi cha Nyanza Mines kilichopo wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma kuongeza
uzalishaji pamoja na kupanua wigo wa soko la ndani ili serikali iweze kunufaika
na uwekezaji huo.
Prof. Riziki Shemdoe
alisema hayo mara baada ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea shughuli za
uzalishaji ambapo amesema lengo la ziara yake ni kutekeleza maagizo ya Raisi wa
Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati wa
kampeni zake katika wilaya hiyo.
Alisema uwekezaji
unaofanyika katika kiwanda hicho ni mkubwa na soko kubwa likiwa nchi Jirani ya
Congo DRC na Burundi kwa asilimia 60 na asilimia 40 ikiwa ni soko la ndani ni
lazima serikali inufaike na uwekezaji huo huku akiitaka halmashauri kukaa
pamoja na kufikia muafaka wa utoaji wa tozo zilizopo kisheria.
“Kwa sasa kiwanda hiki
kinazalisha tani elfu 20 hadi 25 lakini lengo lilikuwa ni uzalishaji wa tani
elfu 50 ambayo haijafikiwa kutokana na changamoto ya mafuriko kutoka katika mto
malagalasi na kusababisha shughuli za uzalishaji kusimama” aliongeza Prof.
Shemdoe.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na waandishi wa habari wakati akikagua kiwanda cha Chumvi Uvinza. (Picha Zote Na Mwajabu Kigaza) |
Weja Ng’olo ambaye ni
mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Uvinza alieleza kutokuwepo kwa
ushirikiano baina ya halmashauri na kiwanda na hilo linachangiwa na kutokuwepo
kwa uwazi wa kiasi kinachokusanywa ambapo hali hiyo inachangia kurudisha nyuma
shighuli za maendeleo.
“ Tozo zilizopo zipo kisheria wanatakiwa kuilipa halmashauri kiasi cha 0.3 ya ushuru wa huduma lakini pia ushiriki wa miradi ya maendeleo kwenye jamii umekuwa ni mdogo mpaka kusukumwa na kwa mwaka wanalipa kiasi kisichozidi milioni 10 , ninachoshauri tu wawe wawazi na walipe tozo zoto ambazo zipo kisheria” alisema Weja.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe akiwa na meneja wa kiwanda cha chumvi Uvinza Boniphace Mwaipopo wakati akikagua kiwanda hicho.
Emmanuel Miselya
kutoka mamlaka ya maendeleo ya biashara Tanzania Tan tred akaeleza namna
ambavyo watahakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi
unaongezeka lakini pia ameeleza sambamba na hilo watahakikisha wanatoa ushauri
kwa kiwanda hicho kuhakikisha soko linakuwa zaidi.
Aidha meneja wa
kiwanda hicho Boniphace Mwaipopo ameeleza licha ya kutoa ajira ya zaidi ya 500
kwa jamii inayozunguka wilaya ya Uvinza lakini bado kuna changamoto kubwa ya
uharibifu wa miundombinu ya kiwanda hicho jambo linalochangia kusimama kwa
shughuli za uzalishaji kwa muda ili kupata vifaa vipya ambavyo vimekuwa vikiharibiwa
na jamii inayozunguka kkiwanda hicho.
Idd Kimondo ni
miongoni mwa vibarua ambapo ameeleza kuwa kiwanda hicho kimekuwa msaada mkubwa
kwao katika kukuza uchumi wao kwenye familia lakini pia kujiepusha na vitendo
vibaya mtaani ikiwemo wizi na uvutaji wa bangi huku baadhi ya kinamama nao
wakipata fedha za kusomesha watoto wao.
Baadhi ya vibarua katika kiwanda cha chumvi Uvinza wakiendelea na shughuri. |
0 Comments