Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Katika mwaka 2019/2020, Serikali kupitia Programu ya Uendelezaji
wa Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) katika fedha zake za maendeleo
pamoja na mambo mengine ilitenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya
mashamba ya utafiti na uzalishaji wa mbegu bora kwa lengo la kuchangia
upatikanaji wa mbegu bora ili kukidhi mahitaji ya Wakala wa Mbegu (ASA),
Makampuni binafsi yanayohitaji mbegu za awali kutoka TARI, na hatimaye
kusambazwa kwa wakulima.
Mwaka 2019/2020, Serikali imetoa fedha za kuweza kununua
matrekta saba (7) na zana zake ambazo zitatumika katika kupanua mashamba ya
uzalishaji wa mbegu na miche bora ya mazao na pia kuimarisha mashamba ya
utafiti kwa kuzalisha aina mpya za mbegu bora za mazao mbalimbali.
Wizara ya Kilimo, kupitia ASDP II imeendelea kuimarisha
mazao ya Kimkakati ikiwa ni pamoja na Michikichi, Korosho, Pamba, Ngano,
Mkonge, Alizeti, Mahindi, Mtama, Uwele na Zabibu. Aidha, Mikakati hii ya Wizara
chini ya ASDP II imechagiwa zaidi na msisitizo wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa
Kassimu Majaliwa Majaliwa ambaye amehamasisha uzalishaji wa kilimo cha
Michikichi na Mkonge hapa nchini. Katika uhamasishaji huo, Wizara kupitia TARI
imeweza kuzalisha miche milioni 2 kwa mwaka 2019/2020 na inategemea kufikia
miche milioni 41 mwaka 2025.
Waziri wa Kilimo
Japhet Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 1 Septemba 2020 katika eneo la Makutupora
Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Matrekta na zana zake ili kuimarisha
uzalishaji wa mbegu unaofanywa na Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI)
na kuongeza kuwa hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali zitakidhi mahitaji ya
mbegu nchini.
Amesema kuwa Matreka hayo
yaliyozinduliwa yamelengwa kuongeza uwezo wa TARI katika kuzalisha mbegu
bora kutoka takribani tani 1,000 kwa sasa hadi kufikia tani 10,000 mwaka 2025.
Vile vile, katika kipindi hicho, TARI itaweza kuzalisha miche kutoka milioni
10.3 ya sasa hadi kufikia miche milioni 40 mwaka 2025.
Waziri Hasunga amesema
kuwa upatikanaji wa matrekta hayo utaimarisha upatikanaji wa mbegu mbalimbali
ikiwemo mbegu za Michikichi zitakazoiwezesha serikali kuwa na utoshelevu wa
mafuta ya kula.
Ameongeza kuwa ili
kuwe na usalama wa chakula ni lazima msisitizo mkubwa uwekwe kwenye
usimamizi madhubuti kwenye sekta ya mbegu ili kuwe na mbegu bora za kutosha na
zenye bei nafuu kwa wananchi.
Waziri Hasunga amesema
kuwa Serikali imekusudia kuongeza uzalishaji wa mbegu mbalimbali za nafaka,
Mboga na matunda kadhalika mazao ya mafuta
Hasunga amesema kuwa
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kuhakiisha inaongeza juhudi za
kuchakata mazao yatokanayo na kilimo ili kuongeza thamani ya mazao na hatimaye
kuimarisha upatikanaji wa malighafi za viwandani.
0 Comments