KIWANDA CHA CHAI MPONDE KUANZA UZALISHAJI



Na Mwandishi Wetu Lushoto


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa chai wilayani Lushoto wajiandae na kilimo hicho kwa kuwa kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo  katika jimbo la Bumbuli kinatarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni baada ya kusimama kwa muda mrefu.

 

Kiwanda cha chai Mponde ni miongoni mwa viwanda vya kusindika majani mabichi ya chai katika Halmashauri ya Bumbuli na hutegemewa na wakulima wadogo wa chai wapatao 5,000 kama soko la majani mabichi ya chai kutoka katika mashamba yao, ambapo uzalishaji ulisimama kufuatia mgogoro uliojitokeza mwaka 2013.

 

Mheshimiwa Majaliwa alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Oktoba 9, 2020) alipozungumza na wananchi wa jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto, Tanga katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Soni wakati alipomuombea  kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli na wagombea udiwani  baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo January Makamba kupita bila ya kupingwa.


 

“Najua msimu huu mmehangaika sana, lazima kiwanda chetu kianze kazi na hatua zote za msingi zimeshakamilika. Msimamizi mkuu ni Msajili wa Hazina na mwekezaji ni mifuko ya hifadhi ya jamiii ya PSSSF na WCF, ambao walishakuja kufanya ukaguzi ila kuna mitambo inahitaji vipuri na tumeagiza vichongwe ili kazi ianze chai isindikwe.”

 

Alisema mitambo ile ni ya miaka mingi sana  na hata teknolojia yake imepitwa na wakati, hivyo kwa sasa wameagiza vipuri vichongwe ili chai ya wakulima iendelee kusindikwa wakati wawekezaji hao wakitafuta mashine nyingine mpya na za kisasa ambazo zitakapopatikana zitabadilishwa huku zoezi la usindikaji likiwa linaendelea.

 

Mheshimiwa Majaliwa alisema mpango wa kibiashara (Business Plan) wa kukarabati kiwanda hicho uliandaliwa na umeshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kama sehemu ya matakwa ya wizara ili kuridhia matumizi ya fedha kutoka kwenye mifuko hiyo kiasi cha shilingi bilioni 4.05 kwa ajili ya ukarabati na uendeshaji wa kiwanda.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments