UPASUAJI WA KISASA WALETA AHUENI KWA WAGONJWA

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Upasuaji wa kisasa wa kuondoa uvimbe wa saratani pasipo kuondoa titi lote lililoathirika umeleta ahueni kwa wagonjwa na kupunguza unyanyapaa kwa wanawake nchini.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Julius Mwaiselage alieleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalum, kuhusu mwezi Oktoba ambao ni maalum Kidunia kwa ajili ya uelimishaji, uhamasishaji, uchunguzi na matibabu ya saratani hiyo.

 

Mashujaa (wanawake waliotibiwa na kupona saratani ya matiti) na wale wanaoendelea na matibabu dhidi ya saratani hiyo, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk. Julius Mwaiselage na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa wakiinua mkono juu kama ishara ya kuishinda saratani hiyo kwa matibabu.

Alisema wastani wa wanawake 100 wanaogundulika na saratani hiyo ikiwa katika hatua za awali, huondolewa uvimbe kwa njia ya upasuaji pasipo kung’olewa titi lote lililoathiriwa kila mwaka ambapo huduma hiyo ilianza kutolewa rasmi mwaka 2016 nchini na wataalamu wa ORCI wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH- Mloganzila).

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk. Julius Mwaiselage akizungumza.

Dk. Mwaiselage amebainisha kwamba ORCI kila mwaka huona wagonjwa wa saratani ya matiti kati ya 600 hadi 700 ambapo hao 100 ambao ni sawa na asilimia 30 hutibiwa kwa kuondoa uvimbe pasipo kung’oa titi lote.

 

“Zamani kwa kuwa hatukuwa na mashine za kisasa za tiba mionzi, matibabu yalikuwa ni lazima kuondoa titi lote, changamoto nyingine tuliyokuwa tunakabiliana nayo ni wagonjwa hawa kuchelewa kuja hospitalini, wanakuja ugonjwa ukiwa umefikia hatua za juu mno, haikuwa rahisi kupata matokeo mazuri ya tiba.

 

“Lakini kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa kutumia mashine hii ya ‘Linear accelerator’, tunao uwezo wa kuchunguza na kutibu kwa kuondoa ule uvimbe tu na kuliacha titi, baada ya upasuaji huo mgonjwa anaendelea na matibabu ya mionzi kupitia mashine ya kisasa tuliyonayo hapa ORCI,” amesisitiza.

 

Aidha alisema kuwa kwa wale waliofanyiwa upasuaji na kuondolewa titi lote jitihada zinafanyika ambapo tayari wataalamu wapo nchini China wakijifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza matiti.

 

Amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kila mwaka Tanzania kuna wagonjwa wapya 42,000 wa saratani aina zote, saratani ya matiti inaongoza duniani kote kwa kuathiri wanawake kwa asilimia 99, wanaume asilimia moja huku takwimu hiyo ikiongezeka kwa kasi.

 

Post a Comment

0 Comments