Na Mwajabu Hoza
MKURUGENZI wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Mwailwa Pangani amewataka madiwani wote
waliokabidhiwa hati ya kuchaguliwa kuwa madiwani katika uchaguzi mkuu
uliofanyika octoba 28 ya mwaka huu kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa
mapato ya halmashauri hiyo kutoka katika vyanzo vilivyopo kwenye kata zao
pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Akizungumza mara baada
ya kukabidhi hati hizo kwa madiwani wapatao 19 Mwailwa Pangani amesema ili
halmashauri hiyo iweze kusonga mbele katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo ni lazima madiwani wawajibike ipasavyo katika suala zima la ukusanyaji
wa mapato lakini pia kusimamia vyema miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.
“ Baraza la madiwani
lililopita madiwani wengi walikuwa wakidai stahiki zao na hilo linatokana na
kusuasua kwa ukusanyaji wa mapato hivyo baraza hili kwa kuwa wote ni wamoja na wanasimamia
ilani ya chama chao ni wazi kuwa watakusanya mapato na wasitegemee kuwa
manispaa kuna hela wanakuja kunufaika hapana bali wao wanatakiwa kuiletea
halmshauri hela kutoka katika vyanzo walivyonavyo” amesema
Baadhi ya madiwani hao
wameeleza ambavyo watawajibika kusimamia vyema utekelezaji wa ilani ya chama
cha Mapinduzi CCM kupitia vipaumbele ambavyo wameviainisha ili
kuhakikisha wanatekeleza miradi yote kwa ufanisi sanjari na wanaondoa
tatizo la upatikanaji wa hati chafu kwa halmashauri hiyo.
Sharon Mashanya ,
Abdallah Kiyembe na Mussa Maulidi kwa nyakati tofauti wamesema vipaimbele vyao
vya kwanza ni pamoja na miundombinu ya barabara na madaraja, vifaa kwa
ajili ya sekta ya afya, kufufua masoko pamoja na kuongeza mitaji kwa vijana,
wanawake na walemavu sanjari na kushawishi uwekezaji ndani ya manispaa hiyo.
Kwa muda mrefu baraza
la halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji limekuwa ikiongozwa na upinzani
ambapo kwa sasa baraza hilo litaongozwa na chama cha Mapinduzi CCM mara baada
ya kuchukua kata 18 kati ya kata 19 zilizopo katika halmashauri hiyo.
Mwisho.
0 Comments