Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma ACP James Manyama |
Na Emmanuel Matinde
JESHI la polisi mkoani
Kigoma limewakamata watu wanne raia wa nchi jirani ya Burundi kwa tuhuma za
kujihusisha na kilimo cha madawa ya kulevya aina ya bangi katika hifadhi ya
Wanyama pori ya Moyowosi kando ya Mto Malagarasi wilayani Kibondo kinyume cha
sheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kigoma ACP James Manyama, alisema, Novemba 8 mwaka huu wakishirikiana na
vyombo vya ulinzi na usalama na idara mbalimbali za serikali, waliwakamata watu
hao wakiwa katika mashamba yao ya bangi yenye ukubwa wa ekari 5 ambayo bado
haijavunwa na magunia saba ya bangi iliyovunwa yenye uzito wa kilo 134.
Aidha Kamanda Manyama
alisema madawa ya kulevya yana athari kubwa kwa jamii ikiwemo kuchochea
ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili, ongezeko la wategemezi, pia huchangia
ongezeko la vitendo vya uhalifu, hivyo polisi wataendelea na operesheni za
kuwasaka wote wanaojihusisha na kulima au kuuza madawa ya kulevya.
Hata hivyo Kamanda
Manyama alisema polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kama kuna
watanzania walioshirikiana na watuhumiwa hao na hatua za kisheria ziweze
kuchukuliwa dhidi yao.
0 Comments