UKOSEFU WA MITAJI NA UOGA VYAWAKWAMISHA WAJASIRIAMALI KATIKA ZABUNI

 


Na Emmanuel Matinde, Kigoma

Imeelezwa kuwa ukosefu wa mitaji, uoga wa kuthubutu ni miongoni mwa vikwazo kwa wajasiriamali wanawake wa mkoa wa Kigoma kushindana katika zabuni mbali mbali zinazotolewa serikalini.

Hayo yalielezwa na baadhi ya wanawake wajasiriamali wa mkoa wa Kigoma, katika mahojiano na Blog hii, ambapo pia walisema changamoto nyingine ni upatikanaji wa taarifa, ukosefu wa elimu na uelewa kuhusu zabuni zinazotolewa na serikali.

“Serikali kweli sasahivi imeamua kutoa kipaumbele kwa wanawake  kutoa mitaji lakini kusema ukweli mitaji bado haijawafikia wale wajasiliamali haswa ambao biashara zao ni kubeba mabeseni ya mihogo, viazi na karanga  ambao hao ndio walikuwa wanalengwa na serikali, lakini pesa hizo zinaenda kwa wale ambao wanajiweza kifedha

Aidha Afisa Manunuzi na Ugavi wa Mkoa wa Kigoma, Baraka Baligumya, alisema kwa kutumia mashirika yasiyo ya kiserikali wanawake wanaendelea kupatiwa elimu ili waweze kupata uelewa wa kutosha na hatimaye kuwania fursa za zabuni serikalini, pia akibainisha kuwa kundi la wanawake ni moja ya makundi maalum ambayo sheria inawapa fursa ya kuchukua zabuni za serikali.

“Kutokana na sheria ya manunuzi namba 9 ya mwaka 2013 imewapa upendeleo watu wa kutoka makundi maalumu wakiwemo wanawake ikiwa ni upendeleo wa 30% na kwa katika kila tenda zinazojitokeza 30% wawe ni watu wanaotoka katika makundi maaluamu hasa wanawake” alisema Baligumya.

Kwa mujibu wa Afisa Manunuzi na Ugavi wa Mkoa wa Kigoma, hali ya wanawake kujitokeza katika zabuni za serikali iko chini ya wastani na moja ya sababu ni kutosajili vikundi.

 


Post a Comment

0 Comments