Na Mwandishi Wetu,
Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote
nchini wafanye ukaguzi kwenye viwanda vya kuzalisha saruji, mawakala,
wauzaji wa kati na wadogo wa bidhaa hiyo na wachukue hatua stahiki.
Alitoa agizo hilo jana (Jumamosi, Novemba 21, 2020) wakati
akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhusu tatizo la kupanda kwa bei
ya saruji nchini kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video
conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, Dodoma.
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa mikoa kwa njia ya Video.
“Wakuu wa Mikoa na Kamati zenu za Ulinzi na Usalama fanyeni
ukaguzi kwa mawakala, ukikuta wamerundika saruji kamata na kuwashtaki. Nendeni
pia kwa wauzaji wa kati, nao pia chekini maghala yao,” amesema.
“Piteni kwa maafisa biashara na muwasimamie iwe ni kwenye
Sekretarieti za Mikoa au katika Halmashauri zenu, tunataka bei irudi kama
ilivyokuwa mwezi Septemba kwa sababu hakuna badiliko lolote kwenye tozo ya
kodi,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ambaye aliitisha kikao cha kwanza na Wakuu hao wa
Mikoa tangu aapishwe, amesema: “Wakati wa uapisho, Novemba 16, mwaka huu nilitambulisha
tatizo la kupatikana saruji kwa bei ya juu sana. Niliagiza kila Mkuu wa Mkoa
afuatilie ni kwa nini bei imepanda kiasi hicho.”
“Nimepokea taarifa zenu na kuona hali halisi iliyoko kwenye
mikoa yenu. Hali si nzuri, akiba iliyopo ni ndogo na bei ni ya juu sana. Nasema
bei ni ya juu sababu tunaangalia bei ya mlaji kwa sasa. Awali ilikuwa kati ya
sh. 14,000 hadi 15,000 lakini sasa hivi imefikia sh. 24,000 kwa mfuko mmoja,”
amesema.
Amesema hiyo ni tofauti ya sh. 9,000 hadi 10,000 lakini kwa sasa
ni lazima bei ishuke kwa sababu hakuna tozo za kodi zilizoongezeka. “Kuna watu
wanatumia kigezo cha gharama za usafirishaji, hii si kweli kwani hata Septemba,
walikuwa wakisafirisha bidhaa hiyo kwa njia zetu zilezile.”
Amewaagiza Wakurugenzi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pia
wakutane na wenye viwanda na kuweka ratiba ya mwaka ili kuepuka viwanda vingi
kufungwa kwa matengenezo ya mwaka kwa wakati mmoja na kufanya saruji iadimike
na kupandisha ghafla bei ya saruji.
Kwa upande wao, Wakuu hao wa Mikoa, wamesema wamepokea maelekezo na
watayatekeleza.
0 Comments