WAZIRI MKUU ATOA SIKU 15 KUKAMILIKA KWA UJENZI WA HOSPITAL YA UHURU


 

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa hospitali ya Uhuru katika Halmashauri ya Chamwino


Na Mwandishi Wetu, Chamwino

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kwa uongozi wa Wilaya ya Chamwino, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Suma JKT wahakikishe ujenzi wa hospitali ya Uhuru katika Halmashauri ya Chamwino unakamilika.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu alisema lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inazinduliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ifikapo Desemba 9, mwaka huu ili kutimiza maono yake ya ujenzi wa hospitali hiyo.

“Nimeridhika na hatua hii ya ujenzi lakini haitoshi, hamieni hapa, huu ni wakati wa kazi, hakikikisheni kazi inafanyika usiku na mchana ili Desemba 5, 2020 kazi ikamilike na Desemba 9, 2020 izinduliwe”

Hospitali ya Uhuru katika Halmashauri ya Chamwino ikiendelea kujengwa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa anataka kuona vifaa vyote vya ujenzi wa hospitali hiyo vinatoka kwenye viwanda vya ndani ili kuharakisha ukamilishwaji wa hospitali hiyo hasa marumaru kwani tayari tuna viwanda vikubwa vinavyozalisha bidhaa hiyo kwa ubora wa hali ya juu. 

“Mnabishana kuhusu uwekaji wa tiles, mnataka za nje? TBA mnang’ang’ania kununua tiles kutoka nje ya nchi, kwa nini? Sisi tumehamasisha ujenzi wa viwanda na viwanda vipo vinavyotengeneza tiles tena nzuri, tuna kiwanda Chalinze kikubwa sana na kingine kipo Mkuranga, hata jengo letu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi tumeweka tiles za ndani, na bora mshitiri hujazinunua, na usinunue kutoka nje, tuna viwanda vipo nchini,” alisisitiza.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMSEMI), Mhandisi Joseph Nyamhaga alisema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Magufuli alilolitoa kuwa kiasi cha sh. milioni 995.1 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru mwaka 2018 zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo. Pia, Januari 2019, wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya simu ya Airtel, aliagiza kiasi cha sh. bilioni 2.415 zitumike kwenye ujenzi huo.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Laurence Lukema alisema wao kama wakandarasi wa ujenzi, watahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments