Na Mathias Canal, Wazo Huru-Dodoma
Serikali imeeleza dhamira yake ya kuanza uchimbaji wa makaa ya
mawe kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko ameeleza mpango huo wa serikali
wakati akizungumza kwenye kikao kazi na watumishi wote wa Wizara hiyo kilichofanyika
katika Mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma tarehe 11 Disemba 2020.
Katika kikao kazi hicho kilichochagizwa na mapokezi ya Naibu
Waziri wa Madini Mhe Prof Shukrani Manya, Waziri Biteko amebainisha kuwa
changamoto na mvutano uliopo baina ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) unapaswa kufika ukomo ili shughuli za
uchimbaji makaa ya mawe uweze kusonga mbele.
Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na watumishi wa Wizara ya Madini kilichofanyika katika Mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma tarehe 11 Disemba 2020.
Amesema kuwa viongozi wote wa Wizara ya Madini wanapaswa
kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha dhamira hiyo ya serikali kwa maslahi
makubwa na manufaa ya wananchi.
“Tutakuwa na urafiki mahali tutakapokuwa tunafanya vizuri na
kununiana pale ambapo hatutafanya vizuri na mimi kiu yangu ni kuona wote
tunafanikiwa” Amesema Biteko
Awali Waziri Biteko amewaasa watendaji wa Wizara hiyo ya Madini
kubadilika kutokana na mazingira kwani mazoea waliyokuwa nayo kabla ya uteuzi
wa Naibu Waziri yanapaswa kumalizika na kulinda heshima ya viongozi hao.
“Mazoea sio mahala pake kwa sasa, na mkiona Mhe Rais amemteua
kiongozi kutoka kwenye Wizara ya Madini maana yake ameona utendaji uliotukaka
kwani ana watanzania wengi wenye uwezo wa kufanya kazi kwa weledi lakini wakati
mwingine anatoa upendeleo” Amekaririwa Mhe Biteko
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini Mhe Prof Shukrani Manya
amesema kuwa matokeo mazuri ya ufanyaji kazi wa watendaji wa Wizara ya Madini
ndio umempatia ngazi ya kupanda daraja hivyo amewataka kuongeza bidii na
ufanisi katika kazi ili kufikia adhma ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa
na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Naibu Waziri wa Madini Mhe Prof Shukrani Manya akizungumza wakati wa kikao kazi na watumishi wa Wizara ya Madini kilichofanyika katika Mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma tarehe 11 Disemba 2020. |
Mhe Manya amewasisitiza watumishi wote kuendeleza ushirikiano ili kufikia dhamira ya ilani ya uchaguzi ya CCM 2020/2025 pamoja na mikakati madhubuti ambayo wizara na taasisi zake imejiwekea.
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Madini wakifuatilia kikao kazi kilichofanyika katika Mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma tarehe 11 Disemba 2020. |
0 Comments