Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la hifadhi za Taifa
nchini (TANAPA) limesema litaanza kutoa tuzo kwa klabu za waandishi wa habari
nchini ambazo zitaandika habari zenye lengo la kutangaza uhifadhi na Utalii
nchini.
Naibu katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii , Dk. Allan Kijazi aliyasema hayo jijini Dodoma wakati
akifunga mkutano wa wahariri, viongozi wa taasisi za kihabari na waandishi wa
habari waandamizi kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Kamishna wa Uhifadhi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Allan Kijazi akifunga mkutano wa wahariri na waandishi waandamizi Tanzania, mkutano uliofanyika jijini Dodoma. |
Alisema, awali walikuwa wakitoa
tuzo kwa waandishi waliofanya vizuri lakini kulitokea tatizo, tuzo zikasitishwa
lakini kuanzia mwakani wataanza kutoa kwa club za waandishi, ambazo waandishi
wake watafanya vizuri.
Aidha alisema kuwa,tuzo hizo
zitaanza kutolewa ikiwa ni mchango wa kuthamini kazi zitakazokuwa zimefanywa na
vyama vya wàndishi wa habari (press clubs)
Aliongeza kwa kuwataka viongozi kuwahamasisha waandishi kwenye
maeneo yao kuandika habari za uhifadhi na Utalii kwa wingi ili kuelimisha jamii
na kutangaza vivutio vilivyopo nchini.
Kwa upande wake Rais wa Muungano
wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Deogratius Nsokolo alilishukuru
Shirika la Hifadhi za Taifa nchini kwa kuendelea kutambua umuhimu wa waandishi
wa habari nchini na kuzitumia press club kuhamasisha shughuli za uhifadhi.
Alisema UTPC ipo tayari
kushirikiana na TANAPA katika ulinzi wa raslimali za Taifa na uhamasishaji wa
shughuli za shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Utalii wa ndani na nje
pamoja na kukabiliana na ujangili.
Alifafanua kuwa, kuanzishwa kwa
tuzo hizo kutawasaidia waandishi kubobea katika uandishi wa habari za uhifadhi
na hivyo kuwasaidia wananchi na Taifa kutokana na kuandika habari za kina na
zenye tija.
Hata hivyo Nsokolo alitoa wito
kwa waandishi nchini kutumia fursa hiyo vizuri ili press klabu ziweze
kushindana na kutimiza malengo ya nchi katika uhifadhi.
Shirika la hifadhi za Taifa
nchini Tanapa linasimamia hifadhi 22 nchini.
0 Comments