Wakulima, wasindikaji, wasambazaji na waraji wa mafuta ya mawese wakiwa kwenye mafunzo ya uzalishaji na usindikaji wa mafuta yenye ubora mkoani Kigoma. |
Na Kadislaus
Ezekiel Kigoma.
Zaidi ya wakulima, wasindikaji, wasambazaji na
waraji wa mafuta ya mawese elfu mbili na mia mbili mkoani Kigoma, wamepatiwa
mafunzo ya uzalishaji na usindikaji wa mafuta yenye ubora kwa kuzingatia
viwango bora vya vifungashio ili kuongeza thamani ya mafuta ya mawese.
Mkurugenzi wa udhibiti ubora kutoka shirika la
viwango Tanzania TBS Lazaro Msasalaga alisema mafuta ya mawese yanayozalishwa
hayakidhi viwango vya ubora kutokana na uzalishaji usiozingatia technologia ya
kisasa katika kuchakata mafuta.
Alisema wazalishaji wengi wa mawese wamekuwa
wakitumia njia za asili ambazo si bora na kwamba mafuta mengi yanakuwa na maji
na hivyo kuchangia athali kwa walaji wanaotumia mafuta ya mawese.
Aidha Festo Kapela ambaye ni mkufunzi kutoka
Wizara ya Viwanda na Biashara alieleza mbele ya wachakataji na wakulima wa
mazao ya mafuta kuwa, asilimia 80 ya mafuta yanayotumika nchini hutoka nje ya
nchi na kwamba ikiwa mafuta ya mawese yatapewa ubora tangu kuandaliwa
yataongeza thamani katika soko la ushindani.
"Nchi za Afrika Mashariki na kati
zinategemea sana mafuta ya nje ambapo kama viwanda vitaboreshwa vya kuchakata
mafuta ya mawese na kuongezwa ubora itakuwa fursa kwa wakulima kuongeza pato la
Taifa kupitia soko la mafuta" alisema Kapela.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa TBS Kanda ya Magharibi
Rodney Alananga alisema katika tathimini ambayo imefanyika wamebaini
mafuta ya mawese yanayotumika kutokuwa na ubora unaotakiwa ikitokana na
uzalishaji duni unaofanywa na wakulima.
Hatahivyo baadhi ya wakulima akiwemo Isaya
Rashidi, na Neema Juma ambaye ni mchakataji mafuta ya mawese wameomba serikali
kuwezesha upatikanaji wa vifungashio na kupunguza bei ili kuendana na hali ya
uchumi kwa wakulima.
0 Comments