WANAWAKE WILAYANI KASULU WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA MIUNDOMBINU YA AFYA

 

Na Kadisilaus Ezekiel.

Wanawake wanaojifungua katika kituo cha afya Kigamano katika Halmashauri ya mji wa Kasulu mkoani Kigoma wameiomba serikali kuongeza miundombinu ya afya ya uzazi ikiwemo majengo na vitanda kufuatia ongezeko la wanawake wanaojifungulia kituoni hapo na kupelekea kitanda kimoja kutumiwa na wanawake wawili hadi watatu.

Wakizungumza mara baada ya kutembelewa na mbunge jimbo la Kasulu mjini Prof. Joyce Ndalichako baadhi ya wanawake hao akiwemo Anita Shedrack na Salome Samwely walisema wanahitaji huduma ziboreshwe kituoni hapo sambamba na kupewa elimu ya uzazi ili waweze kuwa salama wao na watoto.

Mbunge wa jimbo la Kasulu Mji Prof Joyce Ndalichako akizungumza na akina mama alipotembelea kituo cha afya cha Kiganamo kilichopo halmashauri ya Kasulu Mji mkoani Kigoma.


Mganga Mfawidhi kituo cha afya Kiganamo Dkt. Khadija Zegega alisema kumekuwa na ongezeko la akinamama wanaofika kujifungua katika kituo hicho hasa baada ya kuboreshwa kwa huduma za msingi ambapo zaidi ya wanawake mia tatu huhudumiwa kwa mwezi.

“Hatua hiyo pia hutokana na huduma bora zinazotolewa na wahudumu, na tutaendelea kutoa huduma bora kwa akina mama ili kulinda afya zao na watoto wao” alisema.
Mbunge wa jimbo la Kasulu Mji Prof Joyce Ndalichako akiwa amebeba mtoto baada ya kutembelea wodi ya wazazi katika kituo cha afya cha Kiganamo kilichopo halmashauri ya Kasulu Mji mkoani Kigoma.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu Bi. Fatna Laay alisema kwa sasa wanampango wa kuboresha majengo yasiyo tumika ili kuongeza majengo na huduma kutokana na mji huo kuwa na kituo cha afya kimoja cha Kiganamo kinachotegemewa na kata zote.

 

“Mpango uliopo ni kurekebisha majengo yasiyotumika ili nayo aanze kutoa huduma jambo litakalotoa nafuu kwa wananchi wanaotumiaa kituo kimoja cha afya” alisema Bi. Fatma.

Naye Mbunge jimbo la Kasulu Mjini Prof. Joyce Ndalichako alieleza kuzifikisha changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo lake hasa ukosefu wa vituo vya afya kwa  serikali kuu  ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na kwamba kata nyingine zitegemee kupata vituo vya afya kama ambavyo ilani ya ccm inavyoeleza katika kuwahudumia wananchi.

Post a Comment

0 Comments