Na Emmanuel Michael Senny
Umoja wa makanisa ya Kipentekoste mkoani Kigoma CPCT
umeitaka serikali kufanya ukaguzi makini unaoshirikisha wananchi ili kudhibiti
njia zote zinazoweza kupelekea ugonjwa wa Corona kuenea kwa kasi huku wakiitaka
serikali kutoa elimu zaidi ya Virusi vya Corona ili wananchi waelewe na
kufahamu njia sahihi za kujikinga na ugonjwa huo
Hayo yalijiri wakati wa maombi ya kuliombea Taifa la
Tanzania ili Mungu aliepushe na ugonjwa hatari wa Corona ambao umeenea duniani
kote.
Akisoma risala kwaniaba ya CPCT, Katibu wa CPCT
ambaye pia ni Askofu Mtaafu na Mchungaji wa Kanisa la PAG Katubuka Michael
Kulwa alisema pili wamefanya mkutano wa maombi maalumu kwaajili ya kuombea mkoa
na nchi ya Tanzania ili Mungu aepushe na virusi vya corona.
Aidha alisema kuwa serikali na vyombo vinavyohusika
wawe na ukaguzi makini kwa wageni na wenyeji wanaoingia na kutoka nchini pia
serikali itoe vifaa vitakavyobaini washukiwa wa ugonjwa huo hatari.
Aliongeza kuwa serikali ni vema ikatoa elimu dalili
na namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona ili iwe rahisi hata endapo mtu ataambukizwa
itakuwa rahisi kutambua na namna ya kutoa taarifa sehemu husika haraka zaidi.
Naye Katibu Tawala Msaidizi
wa Mkoa wa Kigoma akimuwakilisha Katibu Tawala wa mkoa huo Ndg
Vedasto Makota alisema serikali ya mkoa inaendendelea kujidhatiti katika
kukabiliana na ugonjwa huo hasa kuweka vifaa katika maneo yote ya mipakani
ikiwemo viwanja vya ndege.
Aliongeza kwa kuwataka viongozi wa dini kuchukua
hatua za msingi za kuwaelimisha waumini wao kufuata kanuni za afya huku akisema
serikali nayo itaendelea kutoa elimu kwa wananchi wake.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dr.
Saimon alisema sekta ya afya ya mkoa inaendelea kuchukua tahadhali ikiwemo
kutoa elimu kwa wananchi ili wazifahamu dalili za ugonjwa huo ikiwemo njia
sahihi za kujikinga ikiwemo kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka
kila wakati.
0 Comments