KAMPENI YA NYUMBA NI CHOO YAPUNGUZA MAGONJWA YA MLIPUKO KIGOMA

 

Mkuu wa Mkoa Kigoma Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko mkoani Kigoma yaemezidi kuzaa matunda kila kukicha kutokana na kupungua kwa magonjwa ya kuhara na kipindupindu

Hatua hiyo inakuja baada ya serikali ya mkoa kuanzisha kampeni ya Nyumba ni Choo ambalo limekuwa likisimamiwa na wakuu wa wilaya ikiwemo maofisa afya wa wilaya za mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa Kigoma Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye alithibitisha kuwa  utekelezaji wa Kampeni ya  Nyumba ni Choo ndani ya Mkoa huu kwa kipindi cha Miaka mitano iliyopita, imezaa matunda kutokana na  hali  ya uwepo wa vyoo  kwenye kaya   kuongeza.

Kamishina Andengenye alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha kujadili mafanikio ya mradi wa Kampeni ya nyumba ni Choo mkoani hapa ambapo alisema hali ya uwepo wa vyoo imeongezeka kutoka asilimia 73 mwaka 2015 hadi asilimia 99.45 ya  kaya  zote mwaka 2020.

“Lengo kubwa la kampeni hii ni kuhakikisha tunatokomeza magonjwa ya kuhara na kipindupindu  na kwa hali ya muitikio wa kampeni hii ni wazi kuwa siku za usoni magonjwa ya kuhara na kipindupindu hayatasikika mkoani Kigoma” alisema Kamishina Andengenyi

Ameongeza kuwa kwa miaka ya nyuma mkoa huo umekuwa ukisumbuliwa na magonjwa ya kuhara na kipidupindu huku maeneo ambayo yamekuwa yakiathiliwa na magonjwa hayo ni vijiji vilivyopo mwambao wa ziwa Tanganyika.

Aidha Kamishina Andengenye alizungumzia tathmini ya Serikali kuwa imebaini uwepo wa masoko 107 huku kati ya  hayo 69 ndio yenye vyoo bora huku mengine yakiwa hayana miundombinu rafiki kwa ajili ya huduma kwa jamii.

“Nimeagiza vyoo hivyo ambavyo havina huduma bora ya vyoo utekelezaji ufanyike ili vyoo vyote hapa mkoani viwe na vyoo bora jambo litakalo saidia katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko” Aliongezea Kamishina Andengenye.

Kwa Upende wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Simon Chacha, alisema kampeni  ya Nyumba ni choo imesaidia kupungua kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo magonjwa ya kuhara na kipundupindu.

“Kwasasa kesi za magonjwa ya mlipuko zimepungua mkoani hapa, nikimaanisha ujio wa wagonjwa wa kuhara na kipindupindu sio mkubwa kama ilivyokuwa hawali” alisisitiza Dkt Chacha.

 

Post a Comment

0 Comments