Na Mwandishi Wetu, Kigoma
CORONA ni ugonjwa wa Homa kali ya mapafua ambao kwa kitaalamu
unaitwa COVID19 na uligundulika kwa mara ya kwanza nchini China mwishoni mwaka
2019, Ugonjwa huo ulianza kuenea kwa kasi kutoka nchini china na kuingia katika
nchini nyingine duniani.
Wakati Ugonjwa huo ukisumbua nchini nyingi duniani kwa upande
wa Tanzania ulichelewa kuingia ikiwa ni baada ya jitihada madhubuti za
kudhibiti ugonjwa huo zilizowekwa na serikali kupitia wizara ya afya maendeleo
ya jamii, jinsia, wazee na watoto iliyokuwa chini ya Waziri Ummy Mwalimu.
Aidha hata ulipoingia kwa kisa cha kwanza kutangazwa bado
serikali ilimudu kuudhibiti ugonjwa huo, ambapo aliyekuwa Rais wa Tanzania
Hayati John Pombe Magufuri aliwahimiza watanzania kufunga na kuomba kila mmoja
kwa imani yake ili ugonjwa huu utokomee.
Wakati serikali ikiendelea kupambana na ugonjwa huu ikiwemo
kuwahimiza wananchi kufuata kanuni za afya na maelekezo kutoka Wizara ya Afya baadhi
ya wakazi mkoani Kigoma wameonekana kutofahamu dalili za ugonjwa huo huku
wakiitaka serikali kutoa elimu zaidi kwa wananchi sambamba na kurahisisha
upatikanaji wa vitakasa mikono pamoja na barakoa.
Wananchi hao akiwemo Siwema Hamis, John Amran na Sudi Majidi
walisema kuwa kutokujua dalili za ugonjwa huo inawapa wakati mgumu kutoa
taarifa za ugonjwa jambo linaloweza kupelekea ugonjwa kuenea pindi
atakapopatikana mtu mwenye maambukizi wakati jamii haifahamu dalili zake.
“Tunashindwa kutoa taarifa mana kila ukimuangalia mwenzako
unahisi yuko salama ila kama tukifahamu dalili zake itakuwa nafuu kwetu kutoa
taarifa za ugonjwa ikiwemo kukaa mbali na mtu mwenye maambukizo” walisema.
Wakizungumzia njia za kujikinga wananchi hao walisema kuwa
hawafahamu njia za kujikinga japo baadhi yao wanaonekana kufahamu njia za
kujikinga na ugonjwa huo.
“Sisi tunaiangalia serikali, ni vyema ikatuma wataalamu
wakapita mitaani au hata kwenye mikusanyiko ya watu na kutoa elimu ya namna
sahihi ya kujikinga na corona tofauti na hapo tutajikuta tunaambukizana tu bila
kujua na kuanza kufa mmoja mmoja” waliongeza.
Dkt Ambakise Muhiche ni Afisa Afya wa mkoa wa Kigoma kwa
upande wake alisema suala la elimu kwa wananchi linafanyika ikiwemo kusambaza
vipeperushi mitaani na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu vyenye elimu ya kujikinga na ugonjwa huo
ikiwemo dalili zake hivyo wananchi wasome vipeperushi hivyo.
“Elimu inatolewea sana kama nilivyozungumza ila niwashauri tu
wananchi kusikiliza vyombo vya habari ambapo huwa tunakuwa na vipindi vya
kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa huu, lakini pia wananchi waache tabia ya
kusikiliza elimu ambazo zinapotosha kutoka kwa watu ambao sio wataalamu wa
afya.
“Kuhusu dalili za Ugonjwa huu kwa kifupi ni pamoja na
kukohoa, kichwa kuuma pia kuwa na joto kali lakini mafua yasiyo ya kawaida,
ukiona hivyo fika haraka katika vituo vya kutolea huduma za afya” alisema Dkt
Ambakise.
Aidha Dkt Ambakise alisema kuwa njia za kujikinga ni pamoja
na kutenga ndoo ya maji tiririka kwaajili ya kunawa mikono mara kwa mara,
kutumia vitakasa mikono, kufunika pua na kiwiko cha mkono wakati wa kupiga
chafya sambamba na kuepuka kukaa sehemu za mikusanyiko na kama kuna ulazima
basi tuvae bakoa
“Kwa kufuata njia hizo kwa pamoja tunaweza kupambana na
maambukizi ya ugonjwa wa Corona” alisisitiza Ambakise.
0 Comments