Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya Kigoma imewataka wananchi waishio mwambao wa Ziwa Tanganyika kuzingatia usafi wa mazingira yanayowazunguka kwa kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha ili kudhibiti mlipuko wa magonjwa kama vile kipindupindu.
Hayo yanajiri wakati Tanzania ikiendelea na mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakikwamisha shughuri za maendeleo kwa wananchi ambao huchukua muda mwingi kutafuta tiba badala ya kufanya kazi.
Afisa afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Saulo Mshale, alisema vijiji vilivyopo pembezoni mwa ziwa Tanganyika vimekuwa vikiandamwa na magonjwa ya kuhara kutokana na mazingira machafu na kutozingatia kanuni za afya.
“Wananchi wengi wa pembezoni mwa ziwa hawafuati kanuni za afya ikiwemo kuwa na vyoo bora, kutumia maji machafu na kushindwa kuweka mazingira katika hali ya usafi jambo linalosababisha magonjwa ya mlupuko ikiwemo kuhara na kipindupindu hasa kipindi hiki cha mvua” alisema.
Ameongeza kuwa wananchi wamekuwa
wakitumia maji ya ziwa bila ya kuyachemsha, lakini pia wengi wao hawana vyoo
jambo linalowafanya kujisaidia vichakani lakini pia kukaa kwenye mazingira
machafu kwao ni kawaida.
Aidha Mshale alisema kuwa sekta ya afya imetuma wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutembelea kila kaya kwa lengo la kutoa elimu kwa wancnhi na kuhakikisha wananchi wanafuata kanuni za afya.
“Imebidi tufanye hivyo ili kuhakikisha tunatokomeza magonjwa ya mlipuko katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa ziwa kwa kutuma wataalamu” Aliongeza
Kwa upande wao wananchi waishio mwambao wa ziwa Tanganyika wameiomba serikali kuweka mikakati ya kutoa elimu ya namna ya kufuata taratibu za kiafya.
“Huduma za afya zipo lakini sio kwa kiwango kikubwa lakini tumekuwa tukienda katika vituo vya afya tukiwa tayari tuna wagonjwa, sasa ni vyema serikali ikaja kutoaelimu ili tujue tunajikinga vipi na ugonjwa wa kuhara” walisema.
Kwasasa maeneo mengi ya mkoa wa
Kigoma mvua imekuwa ikinyesha kila wakati hivyo kwa maeneo ambayo mazingira ni
machafu kumekuwa na hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko jambo ambalo serikali
imeanza kulifanyia kazi
0 Comments