Na. Adela Madyane, Kigoma.
Wananchi wilayani Kibondo mkoani Kigoma wameshauriwa kulinda
mazingira na kuachana na dhana kwamba kuchoma moto misitu huongeza umri wa
kuishi.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Misitu na Uhifadhi wa Mazingira
wilaya ya Kibondo Bw. Bareth Ng’umbi wakati akizungumzia suala la
uchomaji misitu bila kujali elimu inayotolewa.
Alifafanua kuwa, misitu na uoto wa asili hulinda vyanzo vya maji
utokanao na uharibifu wa mazingira, ili kuondokana na uhaba wa maji na
upatikanaji wa maji salama na safi, ni lazima wananchi waache tabia ya kuchoma
misitu kwa maandalizi ya kilimo na kwa nia nyingine yoyote.
Alisema wilaya ya Kibondo ni miongoni mwa wilaya zilizo na uhaba
wa maji, serikali inajaribu kila namna kuondokana na changamoto hiyo kwa
kuboresha miundombinu ya maji, lakini wananchi badala ya kupanda miti,
wanaharibu uoto wa asili ambao wanategemea.
"Wananchi wanaona jinsi ilivyo ngumu kupata maji safi na
salama ndani ya maeneo yao, ni mashuhuda wazuri kwamba vyanzo vya mito
vinakauka, mazingira yote ni kavu na tupu, lakini wanaendelea kuchoma misitu,
hivi karibuni tutakabiliwa na ukame na kuiacha miundombinu bila maji
”Aliongeza.
Annajesta Paschal mkazi kutoka Kibondo aliwashauri maafisa ugani
wa wilaya kuimarisha utoaji wa elimu ya uhifadhi wa misitu na mazingira kwa wananchi
bila kuchoka.
Alisema hatua zinazofaa zinapaswa kuchukuliwa kwa wananchi ambao
kwa makusudi wanachoma moto na kuharibu mazingira kama sheria ya
mazingira inavyosema.
Kwa upande wake, Matokeo Justine alisisitiza kwamba maafisa
ugani hawapaswi kukaa ofisini, wanapaswa kuzungukia jamii na kutoa elimu juu ya
athari za kuchoma misitu kwa mazingira kwani kwa sasa wakulima wanaandaa
mashamba bondeni, na wanachofanya ni kuchoma moto nyasi na vichaka ili
kurahisha kilimo.
0 Comments