Na Mwajabu Hoza , Kigoma.
IMEELEZWA kuwa
asilimia 58 ya wazazi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma
wananyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miezi sita mfululizo bila kuchanganya
na chakula chochote na idadi kubwa ni wazazi walio katika sekta rasmi za ajira.
Kaimu mratibu wa lishe
Manispaa ya Kigoma Ujiji Pendo Samizi ameeleza kuwa kwa mujibu wa sera na
sheria mzazi anatakiwa kupata likizo ya uzazi ya siku 84 mara baada ya
kujifungua ili aweze kupata fursa ya kunyonyesha lakini pia kulea vyema mtoto
wake.
“Likizo inapokamilika
mzazi anakuwa na ruhusa ya kwenda nyumbani kunyonyesha kwa kipindi hicho cha
miezi sita na lengo ni kuhakikisha mtoto hapatiwi chakula ama maziwa tofauti na
maziwa ya mama yake” .
Mara kadhaa sheria
imekuwa ikiwalenga wale waliopo kwenye ajira rasmi hususan waliopo serikalini
lakini wale waliopo katika sekta binafsi zenye mlengo wa kibiashara
imekuwa vigumu kuzingatia taratibu za unyonyeshaji wa mtoto na wengi wao
wanaanza kuwapatia watoto chakula ama maziwa ya kopo na ya ng’ombe hali ambayo
ni hatari kwa afya ya mtoto.
“Na hii
linachangia wanawake kukosa fursa za ajira katika taasisi na sekta
binafsi wakihofia kupoteza uzalishaji mali kipindi ambacho mama atakuwa
amejifungua na hivyo ajira nyingi zikifanywa na wanaume”amesema
Alisema serikali
inatakiwa kutilia mkazo na kusimamia sheria iliyopo ili watoto wapate haki zao
za kupata lishe iliyobora kutoka mzazi ambapo hili litasaidia kuondoa
changamoto ambazo watoto wanaweza kuzipata endapo hawatanyonya vizuri maziwa ya
wazazi wao.
Pendo alisema endapo mtoto
atakosa maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita mfululizo atakuwa amekosa
baadhi ya virutubisho na kusababisha kupata matatizo ya kiafya ikiwemo njia ya
hewa, upungufu wa damu mwilini, kutokuwa na uwezo wa kiakili darasani lakini
pia kupungua kwa mahusiano ya karibu kati ya mama na mtoto.
Katika hatua za awali
wameendelea kuelimisha jamii, wadau na kuishauri serikali kuangalia namna ya
kusimamia sera na sheria ili kila mtoto anayezaliwa aweze kupata haki ya
kunyonya vizuri ili kuondokana na magonjwa yanayoweza kujitokeza kwa mtoto.
Hata hivyo wanaume nao
wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawasaidia wazazi kuweza
kunyonyesha watoto wao kwa kipindi chote cha miezi sita ikiwa ni pamoja na
kuwapatia lishe bora kabla ya kujifungua na baada ya kujifungua ili waweze kuwa
ma maziwa mengi ya kunyonyesha watoto wao.
0 Comments