Na Mwajabu Hoza, Kigoma
Changamoto ya
miundombinu ya barabara katika kata ya Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
imeelezwa kuwa kikwazo cha wakazi wa kata hiyo kushindwa kufanya shughuli za
uzalishaji mali ikiwemo kilimo na biashara hususan wakati wa masika kutokana na
kukatika kwa miundombinu ya barabara na kusababisha madimbwi ambayo ni hatari
kwa usalama wao.
Wakitoa kero zao mbele
ya mkuu wa Mkoa Kigoma Thobias Andengenye wananchi hao wamesema barabara
zilizopo kwenye kata ya Nguruka ambazo zinaunganisha maeneo mengine zimekuwa
hazipitiki hasa katika kipindi cha masika na hivyo kuiomba serikali kuwatatulia
changamoto hiyo.
Feruzi Shabani ambaye
ni mwenyekiti wa Kitongoji na Wakawaka Kafulila walisema wakati wa masika
barabara hazipitiki na hivyo kusababisha hata shughuli za uzalishaji mali
kukwama, vitongoji kutengenishwa na hivyo kukosa mawasiliano baina ya kitongoji
na kitongoji .
Akizungumzia ujenzi wa
barabara Mhandisi Richard Maganga Kutoka TARURA wilaya ya Uvinza alisema
barabara zinazounganisha kata ya Igalula, Itebula na Mganza zipo katika mkakati
wa ujenzi kwa kipindi cha mwaka 2021/2022.
Alisema barabara hizo
awali zilikuwa zimetengewe kiasi cha shilingi milioni 30 hadi 50 lakini kwa
sasa serikali imetenga milioni 140 kwa ajili ya kuhakikisha barabara ambazo
zinachangamoto zinafanyiwa matengenezo na kuendelea barabara ambazo ni mpya
zilizoibuliwa.
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Uvinza Jackson Mateso alisema hakuna kata ambayo
itabaguliwa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara ikiwemo ujenzi wa
barabara kwa kiwango cha lami kata zote zinahaki sawa ya kupata maendeleo.
0 Comments