SAMAKI NA DAGAA WA ZIWA TANGANYIKA KIGOMA KUPEWA THAMANI

 


Happiness Tesha, Kigoma

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la chakula na kilimo duniani (FAO), linatarajia kutekeleza mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya uvuvi ikiwemo dagaa na samaki aina ya mgebuka katika ziwa Tanganyika, hali itakayosaidia kupunguza upotevu wa mazao hayo.

Akizungumza  kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na uvuvi , Mkurugenzi wa ukuzaji viumbe maji, Dkt Nazael Madalla katika mkutano wa wadau wa uvuvi kujadili na kuthibitisha matokeo ya utafiti wa mnyororo wa thamani wa dagaa, samaki wa ziwa Tanganyika na changamoto wanazokabiliana nazo, amesema  hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo.

Amesema kutokana na upotevu huo katika mradi huo wanatarajia kufundisha utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao hayo ikiwemo unga wa dagaa ambao pia itasaidia kupunguza utapia mlo.

Madalla amesema dagaa ndio mazao yanayopotea zaidi kwa asilimia 40 hasa kipindi cha mvua kutokana na kutegemea jua katika ukaukaji wake ili ziweze kwenda sokoni.

Mtaalam wa uvuvi kutoka FAO, Hashim Muumin amesema moja ya lenga mradi huo ni kuimarisha lishe kwa wananchi wa wanaozunguka ziwa Tanganyika ili kuondokana na tatizo la utapia mlo katika jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), amesema mtu akitumia mazao hayo kwasasa hawezi kupata virutubisho vya kutosha vilivyokisudiwa mwilini kutokana na kuandaliwa chini ya kiwango.

Amesema mradi wa FISH4ACP ni wa kipindi cha miaka mitano ambapo umeanza mwaka 2020 na kuhusisha nchi 12 na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya na wizara ya maendeleo ya mashirikiano ya uchumi ya Ujerumani na kutekelezwa na Shirika la kilimo na chakula la Umoja wa Kimataifa (FAO), wenye lengo la kuongea mnyororo wa thamani wa dagaa na migebuka wa ziwa Tanganyika.

Wadau wa Uvuvi wameiomba pamoja na wadau wa maendeleo kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ambao itasaidia kuondokana na changamoto zinazowakabili.

" Tunachangamoto mbalimbali zinazotukabili kama wavuvi na wafanyabiasha,masoko ni tatizo lakini pia hatuna mialo ya kuanikia mazao yetu kama dagaa ndio maana hatuwezi kupata bidhaa bora ukilinganisha maeneo mengine,"amesema Francis Jonh.

 

Post a Comment

0 Comments