Na Mwandishi Wetu Manyoni
Serikali
imesema ipo katika hatua za mwisho za Mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya
mwaka 2003 kwa kushirikiana na wadau na imeendelea kutekeleza afua mbalimbali
zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili Wazee.
Hayo
yamesemwa Wilayani Manyoni Mkoani Singida na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea
Makazi ya Wazee wasiojiweza ya Sukamahela kuelekea Siku ya Wazee Duniani Oktoba
Mosi.
Waziri
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali
katika kuboresha maisha ya wazee hapa nchini ili kuhakikisha wanapata huduma
jumuishi na stahiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, ikiwemo kuboresha
utoaji wa huduma kwa wazee kuwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Ameongeza
kuwa Maadhimisho haya kwa mwaka huu 2021 yatafanyika katika ngazi za mikoa na
yataongozwa na Kauli Mbiu isemayo:“Matumizi Sahihi ya Kidigitali kwa
Ustawi wa Rika Zote”.
"Sherehe
za maadhimisho ya siku ya wazee itahusisha huduma mbalimbali kama vile wazee
kupima presha, kisukari, tezi dume, huduma za msaada wa kisaikolojia na
elimu kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuhamasisha wazee na
wananchi kupata chanjo." alisema Dkt Gwajima
Katika
hatua nyingine Waziri Dkt Gwajima ameiagiza mikoa ya Rukwa na Njombe kuunda
Mabaraza ya Wazee ya Mikoa hiyo ili kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la
Wazee litakalosaidia kuleta wazee pamoja katika mijadala mbalimbali na kuweka
mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Akisoma
taarifa ya Makazi ya Wazee Sukamahela Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo Twaha
Kibalula amesema kuwa Makazi hayo yanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari
kwa ajili ya kutoa huduma kwa Wazee hao ikiwemo huduma za kiafya zinazopatikana
kwenye hospitali za Wilaya na Mkoa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Rahabu Mwigwisa amemshukuru Waziri
Dkt. Gwajima kwa kuwatembelea Wazee hao na amemuhakikishia kuwa Wilaya
itaendelea kuwaangalia kwa ukaribu Wazee hao kwani ni tunu kwa Taifa hivyo
itahakikisha wanapata huduma zote stahiki.
Akitoa
salamu kwa niaba ya Wazee wenzake Mwenyekiti wa Wazee hao Mzee Adrea
Yohana amemshukuru Waziri Dkt Gwajima na Serikali kwa ujumla kwa huduma
wanazozipata na kumuomba kuendelea kuboresha huduma za afya, chakula na malazi
ili waweze kuishi kwa amani na furaha zaidi.
0 Comments