JAMII MKOANI KIGOMA YATAKIWA KUWAPA KIPAUMBELE WALEMAVU

 


Na Mwajabu Hoza, Kigoma

JAMII na ngazi ya familia imetakiwa kuwapa msaada watu wenye ulemavu na kuwashirikisha katika shughuli za kijamii na  sio kuwatenga na kuwaficha majumbani jambo linalochangia kuwapatia msongo wa mawazo pamoja na kushindwa kujitegemea katika maisha yao.

Angela Kilasi mkazi wa Njombe ambaye anazungumzia changamoto hiyo siku ya maadhimisho ya SIDO kitaifa amesema watoto wengi wanaozaliwa na ulemavu wamekuwa wakitengwa na jamii lakini pia familia zimekuwa zikiwanyanyapaa na kutowapa malezi na makuzi mazuri.

Amesema kila mtoto anayezaliwa anakuwa na uwezo wake kiakili lakini pia wanakuwa na vipaji mbalimbali  ambavyo vingewawezesha kujisimamia wao wenyewe pindi wanapokuwa lakini familia nyingi zimekuwa zikiwaficha majumbani bila kuwapatia elimu wala ujuzi jambo linalochangia kuuwa vipaji walivyonavyo.

Angela anaeleza Miaka saba iliyopita alipoteza uwezo wake wa kuona licha ya kuwa alizaliwa akiwa na uwezo wa kuona jambo ambalo lilisababisha mume wake aliyekuwa akiishi naye kumtelekeza na watoto mmoja akiwa wa miezi miwili.

 “ Tukiwa tumetoka hospitali ndani ya gari mume wangu alinambia niende nyumbani kwa wazazi wangu mjini Njombe nikamuuliza kwanini akanambia we nenda kila kitu chako pamoja na nguo vitakuja huko, Niliumia sana kusikia hivyo nikajua utu wangu umeshaondoka”

“Nilifika nyumbani wazazi wangu walinipokea nikiwa na watoto wangu , walihusunika sana na kunipa moyo, sikuwa tayari kuikubali hali yangu nilikaa ndani kwa kipindi cha miaka mitatu nilitamaji kujiuwa mimi na watoto wangu” alisema.

Angela anaeleza kuwa baada ya muda aliizoea hali yake na kuamua kuanza kujishughulisha na kazi ndogondogo ikiwemo kufuma, kutengeneza urembo kwa kutumia shanga, vikapu, mauwa, kuimba nyimbo pamoja na kuandika kitabu cha “Nimepoteza macho si utu”.

“haikuwa rahisi kwangu wakati wa malezi ya mtoto wangu wa miezi miwili kwani mara kadhaa nilijikuwa nikimnyonyesha maeneo ambayo sio sahihi maana wakati mwingine nilinyonyesha miguu ndipo wazazi wangu waliamua kumchukua na kuanza kumpa maziwa ya Kopo” alieleza.

Amesema kwa sasa ameikubali hali yake ambapo pia alipatiwa fimbo ya kutembelea wakati akiendelea kuelimisha watu wengine wenye ulemavu kujishughulisha katika utafutaji wa kipato na kutojinyanyapaa wenyewe akiwa na “KAULI MBIU MTOE MLEMAVU NDANI MJENGE AJITEGEMEE”

Akizungumzia changamoto ya ujifunzaji amesema walemavu wasioona bado wana changamoto kwani wao hutumia maandishi ya nukta hivyo ni vigumu wao kupata vitendea kazi vya kujifunzia lakini pia vitabu ambavyo vinaendana na hali yao waliyonayo “ Nitahakikisha kitabu change kinakuwa kwa njia ya sauti ili kuwawezesha wasioona waweze kujifunza kutoka kwangu “

Anoaliti Muhicha ni mtoto mwenye umri wa miaka 13 ambaye alianza kumsaidia mzazi wake akiwa na umri wa miaka mitano ambapo amesema kabla ya kwenda shule alihakikisha anamuandalia mahitaji yote  yanayohitajika katika kutengeneza bidhaa zake.    

Baadhi ya wananchi wanaeleza kuwa changamoto ya ujifunzaji kwa watu wenye ulemavu wa kutoona bado ni changamoto ambapo serikali inatakiwa kuangalia namna itakavyowawezesha walemavu wa aina hiyo nao waweze kujifunza pamoja na kupatiwa walimu wenye uelewa waweze kuwasaidia.

Wameeleza kuwa ukiachilia mbali hao wanaojifunza kwa maandishi hayo ya nukta lakini pia wale wanaojifunza kwa lugha za alama nao bado wanachangamoto ya upataji wa walimu wazuri wa kufundisha lugha hiyo.



 



Post a Comment

0 Comments