MAWAZIRI KUTEKELEZA MAAGIZO YA RAIS KUHUSU MATUMIZI YA TSH. 1.3 TRILIONI

 


Na Mwandishi Wetu, Dodoma. 

Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu fedha Sh1.3 trilioni za Mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, imewaibua Mawaziri wakishusha rungu kwa Watendaji.

Mwishoni mwa wiki Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia matumizi ya fedha hizo na kutoa onyo kama watu wanataka kujua rangi yake basi wachezee fedha hizo.

Fedha hizo zimeelekezwa kujenga madarasa vyumba vya madarasa 15,000 ambapo Tamisemi imesema kati ya hivyo, 12,000 vitakuwa vya Sekondari.

Nyingine Ujenzi wa majengo ya huduma za dharura na vyumba vya wagonjwa mahututi na ununuzi wa vifaa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Ummy Mwalimu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amesema miradi yote inayogusa fedha hizo itakuwa na kipimo kwa watumishi wa Serikali na atakayekwenda kinyume ajiandae kushughulikiwa.

Mchengerwa amesema kuanzia sasa kila mtu anatakiwa kukimbia na siyo kwenda mwendo wa kinyonga kwani fedha hizo zinatakiwa kukamilisha miradi yake ndani ya miezi tisa tu.

Ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) waamke ili wafuatilie miradi hiyo kuanzia hatua za mwanzo na bila kuwaonea huruma.

"Watumishi watapimwa kupitia fedha hizi, hakuna shilingi itakayopotea vinginevyo hatavumiliwa mtu katika hili,wasimamizi waamke na waongeze umakini zaidi," amesema Mchengerwa.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ummy Mwalimu ameagiza miradi yote itakayojengwa kupitia fedha hizo iandikwe jina la mradi wa Uviko-19.

Ummy meyasema hay oleo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari, akitaja sababu za kuandika miradi hiyo kuwa ni uchakachuaji unaofanyika kwenye miradi hiyo.

Waziri Ummy amewaagiza Wakurugenzi Tamisemi kugawana mikoa ya kusimamia miradi hiyo na kila mmoja atakuwa akitoa taarifa kila baada ya wiki mbili wakati Waziri na Naibu wake watakuwa wakizunguka wilayani kuhimiza Ujenzi.

 

Post a Comment

0 Comments