TAKUKURU KUSHUGHURIKIA MIRADI 41 ILIYOKATALIWA NA MBIO ZA MWENGE


Na Mwandishi Wetu, Geita

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama, amesema jumla ya miradi ya maendeleo 1,067 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 katika sekta mbalimbali imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi  nchini kote, wakati wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru zilizokimbizwa kwa takribani miezi mitano.

Waziri Mhagama aliyasema hayo katika uwanja wa Magufuli wilayani Chato mkoani Geita wakati wa kilele cha mbio maalum za Mwenge wa  Uhuru, kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha wiki ya Vijana kitaifa.

Alisema wakati wa mbio zake, Mwenge wa Uhuru umekataa kuzindua ama kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 41 iliyopo katika wilaya 38 nchini, kutokana na miradi hiyo kuwa na dosari mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa harufu ya rushwa kwenye miradi hiyo.

Aidha Waziri Mhagama alisema tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imekabidhiwa taarifa za miradi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi, na wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu watachukuliwa hatua za kisheria.

Sambamba na hayo yote Waziri Mhagama alitumia sherehe hizo kutangaza kuwa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 utafanyika mkoani Njombe na kilele cha mbio hizo, kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wiki ya Taifa ya Vijana kitakuwa mkoani Kagera.

 

 

 



Post a Comment

0 Comments