WALEMAVU WAPEWA MSAADA WA VIFAA SAIDIZI

 




Na  Mapuli  Misalaba, Shinyanga

Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo imekabidhi vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu mbalimbali  msaada ambao ulitolewa na mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia kazi vijana na ajira Patrobas Katambi

Jumla ya watu 42 wenye ulemavu wamekabidhiwa  vifaa hivyo katika ofisi za shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA Mkoa wa Shinyanga

Akikabidhi vifaa hivyo kwa wenye ulemavu wa viungo na wasioona Afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Shinyanga Elizabeth Mweyo ametoa  Baiskeli 6 zenye magurudumu matatu za watu wenye ulemavu, fimbo nyeupe 20 kwa ajili ya wasioona pamoja na magongo 16 ya kutembelea, huku akiwasisitiza walengwa kutobadili matumizi yaliyokusudiwa katika  vifaa hivyo

“Kuna baadhi huwa  mnapewa Baiskeli mnaenda kuziuza hamjapewa kwahiyo sababu, mmepewa kwa sababu ya kuwasaidia ziwarahisishie kufanya majukumu yenu ya kila siku kwahiyo msiende kuziuza tutawafuatilia kwa sababu orodha yenu tunayo tutawafuatilia kujua hivyo vifaa mnavitumia, mnazo, zinafanya kazi au mmeshaziuza”

Baada ya kupokea msaada huo baadhi ya watu wenye ulemavu waliopatiwa  vifaa hivyo wamemshukuru mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini  Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi vijana na ajira Patrobas Katambi na serikali kwa ujumla



Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha walemavu Mkoa wa Shinyanga Bwana Mohamed Ally amewataka wale wote waliobahatika kupata msaada huo kuvitunza vifaa hivyo saidizi ili viweze kudumu

Naye mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu  SHIVYAWATA mkoa wa Shinyanga Richard Mpongo  amewaomba  watu wenye ulemavu kushirikiana na vyama vyao vyote pamoja na kujitokeza watu wenye ulemavu ambao hawatambuliki kwenye vyama

Post a Comment

0 Comments