Na Emmanuel Michael, Kigoma
Utoro kwa wanafunzi wa
shule za msingi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma umeelezwa
kuchangiwa na baadhi ya wazazi na walezi kuwatumikisha watoto wao kwenye
shughuli za kilimo wakati wa msimu wa masika.
Kituo hiki kimezunguka
katika baadhi ya shule za msingi kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kigoma ikiwemo
shule ya Msingi Kiganza na kuzungumza na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Said Nshoye
ambaye ameeleza kuwa kipindi cha msimu wa masika wazazi na walezi wamekuwa
wakiwapeleka watoto wao shamba kwa lengo la kuwasaidia shughuli za kilimo.
Amesema tabia hiyo
imekuwa ikichangia utoro wa wanafunzi kila ifikapo msimu wa masika na kuadhiri
maendeleo ya kielemu na hata kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao kushuka
kutokana na kutohudhuria vipindi vya masomo darasani.
Nshoye amesema
changamoto ya utoro inaadhari kubwa kwa wale wa elimu ya awali ambao wanatakiwa
kujua (KKK ) kusoma, kuandika na kuhesabu ikiwa ni msingi wa elimu kwa
wanafunzi jambo linalochangia wanafunzi wengi kiwango chao cha elimu kuwa
chuni.
“Tatizo kubwa ni pale
ambapo wale watoto wenye umri mdogo wanaosoma chekechea hadi darasa la
tatu mara nyingi hubaki nyumbani pale wanapoona dada ama kaka zao hawaji shule
na wao hawaji na hilo linawajengea tabia ya utoro tangu wakiwa wadogo” amesema
Wakizungumza na Blog
hii na baadhi ya wanafunzi akiwemo Ismail Hamza, Ashura Issa wamekiri kuwepo
kwa tabia ya wazazi kuwatumikisha kwenye shughuli za kilimo pamoja na kazi za
nyumbani huku wakiwazuia kwenda shule.
“Wakati wa masika
wazazi wamekuwa wakituzuia kwenda shule ili tukawasaidie shughuli za kilimo
shambani na wakati mwingine tunapewa kazi za nyumbani muda ambao
tunatakiwa kwenda shule kusoma na hilo linasababisha sisi kuwa watoro shuleni”
walisema wanafunzi hao
Wakitoa maoni yao
wananfunzi hao wamesema elimu ni msingi wa maisha hivyo wamewaomba wazazi na
walezi kuwapatia nafasi ya wao kupata fursa ya masomo bila kujali msimu wa
kilimo jambo litakalochangia wao kufikia malengo yao sambamba na wadogo zao
ambao wanasoma elimu ya awali.
Wakizungumzia hilo
wazazi akiwemo Delifina Simon na Astelia Patrick wamesema hakuna ukweli wowote
wa wazazi kuwa chanzo cha watoto kutokwenda shule bali kumekuwa na tabia ya
watoto wenyewe kujificha porini ama kwenda mtoni kuoga jambo linaloathiri hata
wadogo zao wanaosoma elimu ya awali mana wanaona kile wanachofanya wakubwa zao.
“ Watoto wengi ni
waongo wanaaga asubuhi wanaenda shule hawafiki wanaishia maporini kudandia miti
ya matunda na wengine wanakwenda mtoni kuoga hata muda huu ukiingia porini
utawakuta muda ukifika wa kurudi nyumbani nao wanarudi” walisema
Mwenyekiti wa Kijiji
hicho Abel Godfrey amesema suala la kutumikishwa watoto katika kijiji hicho
lilikuwepo ambapo serikali ya kijiji imejipanga kuwachukulia hatua za kisheria
wazazi ambao watabainika kuwatumikisha watoto wao katika shughuli zao za
utafutaji mali katika familia na kutoa wito kwa wazazi, walezi na walimu
kujenga tabia ya mawasiliano ya vikao vya mara kwa mara ili kujua maendeleo ya
elimu kwa watoto wao.
“Ufuatiliaji unatakiwa
kuanzia kwa wale watoto wa elimu ya awali mana ndiko kwenye msingi wa maendeleo
ya mtoto kuipenda shule na kuwa na maendeleo mazuri kielimu” alisema.
0 Comments