MAJALIWA: SERIKALI INAENDELEA KUBORESHA SEKTA YA ELIMU



Na Mwandishi Wetu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita ipo makini na inaendelea kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya elimu ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 27, 2021) wakati akizungumza na walimu, watumishi wa shule na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kayuki baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa manne shuleni hapo akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Rungwe, Mbeya.

“Mheshimiwa Rais Samia ametoa fedha nyingi katika sekta ya elimu ili kuhakikisha shule za msingi na sekondari, vyuo vya elimu ya juu na ya kati vinaboreshwa, hivyo tumieni vizuri miundombinu hii kwa kusoma kwa bidii na mtimize ndoto zenu.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Maofisa Elimu wahakikishe wanatenga muda na kwenda katika shule kwa ajili ya kuzungumza na walimu na wanafunzi na kusikiliza kero zao na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi badala ya kusubiri ziara za viongozi wa Kitaifa.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa maktaba na chumba cha TEHAMA katika chuo cha Ualimu Tukuyu, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini watimize majukumu yao na washughulikie matatizo ya Watanzania ipasavyo.“Tushughulike na matatizo ya wananchi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya hakikisheni miradi yote inayotekelezwa, inakamilika kwa wakati na kwa viwango.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza kila mtumishi wa umma kuwatendea haki Watanzania ikiwa ni pamoja na kuwahudumia katika sekta zote. “Hili ni jukumu letu, tunapaswa kuwa wawajibikaji, tufanye kazi na ziwe za matokeo chanya”

Akiznugmza baada ya kutembelea kiwanda cha Maji cha Tukuyu Spring water Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kuwasaidia wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wadogo ili wafanye vizuri katika shughuli zao kwa kuwa kuna faida kubwa kwa Taifa.

Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka Chuo cha Ufundi Arusha Mhandisi Saidi Shaushi amesema ujenzi wa jengo hilo la maktaba ambao kwa sasa umefikia asilimia 70 unagharimu shilingi milioni 346. Mradi huo unatekelezwa kupitia mfumo wa force account.

 


Post a Comment

0 Comments