ASILIMIA 43 YA WATOTO WANAKABILIWA NA CHANGAMOTO KATIKA UKUAJI

Na Mwajabu Hoza , Kigoma 

WAZIRI wa Afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na  watoto Dorothy Gwajima amesema  asilimia 43 ya watoto nchini Tanzania wapo katika hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji wao kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika makuzi, malezi ya maendeleo ya awali ya ukuaji.

Akimwakilisha Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa uzinduzi wa program Jumuishi  ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto MMMAM wenye  lengo la kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 mpango ambao utatoa fursa ya utekelezaji wa mpango wa  maendeleo ya Taifa wa miaka mitano.

Waziri Gwajima amesema watoto hao wapo katika hatari ya kushindwa kufikia hatua hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo, utapiamlo  umaskini , kukosekana Kwa uhakika wa chakula , miundombinu duni , uhaba wa rasilimali , utelekezwa pamoja na  unyanyasaji  katika jamii na hivyo kuchangia udumavu Kwa watoto hao.

Sambamba na hayo pia kukosekana Kwa uelewa wa kina juu ya  makuzi malezi na maendeleo ya awali ya watoto Kwa wazazi na walezi pia imekuwa ikichangia hali ya ukuaji wa watoto kuwa hatarini hivyo elimu inatakiwa kutolewa kwa wazazi ,walezi na jamii ili watambue vyema utekelezaji wa mpango huo na wao wawe chachu ya mafanikio yenye tija Kwa wanufaika wa mpango.

Akizungumzia hali ya lishe nchini amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi ya chakula na lishe pamoja na ofisi ya takwimu ya Mwaka 2018 

zinaeleza watoto milioni 2.6 wenye umri chini ya miaka mitano wana udumavu licha ya mikoa iliyobainika kuwa na watoto wenye udumavu kuzalisha chakula cha kutosha hivyo hatua zimetakiwa kuchukuliwa ili kuondoa tatizo la udumavu Kwa watoto hao.

Katika kukabiliana na changamoto ya lishe duni Kwa watoto amezitaka halmashauri zote inchini kuhakikisha zinatenga bajeti ya kiasi cha shilingi 1000 Kwa kila mtoto ambayo itachangia upatikanaji wa lishe kwa watoto, huku akitumia fursa hiyo kuhamasisha wajawazito kuhudhuria kliniki Kwa wakati ili kuepusha vifo visivyo vya lazima Kwa watoto pindi wanapozaliwa. 

Mpango huo ambao umezinduliwa leo umekuwa na  matamko kutoka katika wizara zote ambazo zinahusika moja Kwa moja katika utekelezaji wa Programu hiyo ambayo itakuwa chini ya uratibu wa Kisekta kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya na Wadau wote wakiwemo Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha na Mipango ambapo kwa pamoja wametoa matamko mbalimbali yenye lengo Jumuishi la makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto.  

Naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi Hamis Chilo akitoa tamko la Wizara ya mambo ya ndani kupitia Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia amesema wataendelea kumlinda mtoto ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia vitendo vya ukatili ambavyo watoto wamekuwa wakifanyiwa katika jamii  pamoja na kuwataka wazazi , walezi na jamii kutoa ushirikiano katika upatikanaji wa ushahidi kwenye kesi zinazowahusu watoto sambamba na kuacha mila na desturi ambazo zinaathiri saikolojia za watoto.

 Amesema wizara itatekeleza mpango wa Taifa wa malezi , makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Kwa kuzingatia Sera, sheria, mikakati na miongozo Kwa kushirikiana na wizara zingine za Kisekta pamoja na wadau wote wanaohusika katika malezi na makuzi ya watoto .

Katika program hiyo wadau mbalimbali watashiriki wakiwemo TECDEN, na AfECN ambayo ni mitandao ya malezi , makuzi na maendeleo ya awali ya Tanzania , shirika la Afya Duniani

(WHO) , Benki ya Dunia, wafadhili wa MMMAM ambapo  utatekelezwa nchi nzima Kwa kipindi cha miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026.

Baadhi ya wazazi na walezi wameeleza kuunga mkono mpango huo ambao utakuwa na tija katika kumlinda mtoto na kusaidia ukuaji wake na hivyo kuziomba mamlaka husika kusimamia vyema mpango huo ili uweze kuwa na matokeo chanya katika jamii.

 

 

Post a Comment

0 Comments