Na Mwajabu Hoza, Kigoma
HALI ya maambukizi ya
virusi vya Ukimwi mkoani Kigoma imeelezwa kupungua na kufikia asilimi 2.9 jambo
ambalo limeelezwa kuchangiwa na wananchi kujitokeza kupima afya zao na
changamoto ikibaki kwa wanaume kutojitokeza kupima afya.
Taarifa za awali
zinaonyesha hali ya maambukizi ya virusi vya ukimwi ni asilimia 3.4 hali
iliyokuwa ikichangiwa na jamii kutokuwa na uelewa wa kujitokeza kupima ili
kuweza kupata huduma mapema na kupunguza hali ya maambukizi mapya.
Matumizi ya dawa za
kupinguza makali ya virusi vya ukimwi imeelezwa kuendelea kupunguza hali ya
maambukizi kwa mkoa wa Kigoma ambapo wanaojitokeza kwa wingi kupima wamekuwa ni
wanawake.
Hali hii imekuwa
ikichangia baadhi ya wanaume kuamini kuwa wenza wao wakipima inakuwa imetosheleza
na kutoona sababu ya wao kupima jambo ambalo limeelezwa kuwa ni hatari hususani
wakati wenza wao wakiwa na mjamzito.
Taarifa zinaeleza
endapo mama atakuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kuna uwezekano wa
kumuambukiza mtoto kabla na wakati wa kujifungua lakini pia wakati wa
kunyonyesha hivyo ipo sababu ya wazazi kupima afya zao ili kuhakikisha
wanachukua tahadhari za kiafya kwa mtoto anayetarajia kuzaliwa.
Wataalamu wa afya
wanaeleza kuna uwezekano wa mtoto kupata maambukizi kutoka kwa mama akiwa tumboni
na hilo linaweza kujitokeza endapo atuagusishwa na damu ama majimaji kutoka kwa
mama lakini pia wakati wa kunyonya endapo mama atakuwa na vidonda.
Akizungumzia ushiriki
wa wanaume wakati wa siku ya Ukimwi duniani mratibu wa Ukimwi Dkt,Hosea
William amesema licha ya kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya virusi vya
Ukimwi ukilinganisha na mikoa mingine pamoja na ile ya kitaifa ya asilimia 4.7
bado tabia ya wanaume kutopima afya zao imekuwa ikichangia hatari ya afya kwa
wenza wao.
Dkt. Hosea amesema hatua
ya kupungua kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi inatajwa kuwa ni juhudi za
serikali Pamoja na wadau kuhakikisha elimu na umuhimu wa kupima afya kuwa ni
kipaumbele katika mapambano dhidi ya virusi hivyo lakini pia wanaobainika
kuanza kupata dawa mapema.
Staphord Chamgeni na
Dkt,Beatres Mtesigwa wameeleza kuwa bado jitihada zinaendelea za kutoa elimu
kwa jamii hususani wanaume ili kuona umuhimu wa kupima afya zao na kuacha tabia
ya kujinyanyapaa wenyewe.
Asilimia 74.7 ya
wanaume mkoani Kigoma ndio hujitokeza kupima huku wanawake ikiwa ni asilimia
88.7 ambapo wanawake wengi hujitokeza kupima kwa maslahi ya kulinda
familia zao ikiwemo watoto huku wanaume wakibaini kuwa mwanamke anatatizo la
VVU huwa wanawatelekeza wenza wao pamoja na watoto.
0 Comments