Na Mwajabu Hozza, Kigoma
WIZARA ya mifugo na uvuvi imekuwa ikichangia pato la Taifa kwa asilimia 1.7 kiwango ambacho kimeelezwa kuwa kidogo ukilinganisha na rasilimali zilizopo na hivyo wizara kuja na mpango mkakati wa kukabiliana na upotevu wa mazao ya uvuvi pamoja na kuongeza uwekezaji kwenye sekta hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na katibu mkuu wizara ya mifugo na Uvuvi Rashid Tamatamah wakati wa warsha ya wadau wa mradi wa FISH4ACP ambao utaanza 2022 /2024 na umelenga kuboresha mnyororo wa thamani Kwa mazao ya samaki na dagaa.
Amesema katika mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2021 mpaka 2026 sekta ya uvuvi imejipanga kuongeza pato la Taifa na kufikia asilimia tatu kwa kufanya maboresho mbalimbali ikiwemo kuwezesha miundombinu yote inayohusiana na sekta ya Uvuvi , ununuzi wa meli nne pamoja na kuwaunganisha wavuvi na wachakataji wa mazao ya Uvuvi kwenye taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo.
Mkurugenzi wa Uvuvi wizara ya mifugo na uvuvi Ummanuel Bulayi amesema ili mradi wa FISH4ACP uwe na tija lazima wadau wote wa sekta ya uvuvi kushirikiana kwa pamoja kutokomeza uvuvi haramu kwenye maziwa makuu jambo litakalochangia kuwa na uvuvi endelevu katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma .
Aidha Katibu Tawala
mkoa wa Kigoma Rashid Mchatta amesema mradi huo ambao unalenga kanda za
Afrika utakuwa na fursa nzuri ya kuufungua mkoa wa Kigoma kiuchumi
kupitia rasilimali zilizopo.
Baadhi ya washiriki wameeleza changamoto zinazowakabili katika shughuli
zao za uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki na dagaa kuwa ni pamoja na kutokuwepo
kwa bei elekezi za samaki na dagaa pamoja na ukosefu wa masoko na hivyo
kuchangia hali ya kipato kuwa chini huku wakipongeza serikali kwa mradi
uliowafikia ambao utasaidia upatikanaji wa mikopo.
0 Comments