KIGOMA YAZINDUA KAMPENI YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

 


Na  Mwajabu Hoza , Kigoma

Mkoa wa Kigoma umezindua Kampeni ya  kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia itakayo jumuisha wadau mbalimbali watakao iwezesha jamii na mamlaka husika kushirikiana kwa pamoja kutokomeza vitendo hivyo.
 
Kampeni hiyo yenye kauli mbiu isemayo “Twende pamoja ukatili wa kijinsia Kigoma sasa basi” itajumuisha Mkundi kadhaa ikiwemo wanahabari, viongozi wa dini, wasanii na wazee watakaoiwezesha jamii kupata elimu sahihi juu ya vitendo vya ukatili.
 
Kigoma imetajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayotekeleza vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili wa kingono kwa makundi ya wanawake na watoto na matukio mengi yameshindwa kufanyiwa kazi ipasavyo kutokana na matukio hayo  kufanyika ndani ya familia na kuishia kumalizwa kifamilia.

Afisa ustawi wa jamii mkoa wa Kigoma Elisha Nyamala amesema kwa mwaka kumekuwa na matukio ya ukatili kati ya 200 hadi 300 yanaripotiwa kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Kigoma na matukio 1014 yameripotiwa na kati ya hayo 34 yametolewa hukumu wengine wamehukumiwa kifungo cha  maisha na wengine wamehukumuwa kifo.
 
Mkurugenzi idara ya maendeleo ya jamii kutoka wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Mwajuma Magwiza amesema elimu ni miongoni mwa sababu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia ambapo kampeni hiyo itakuwa jumuishi kwa  kwa kushirikisha wadau wa maendeleo , mashirika , asasi , na jamii na lengo ni kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha wanatumia fursa aliyonayo kutoa elimu.
 
Ukiachilia mbali madhara ya kisaikolojia na kimwili kwa mtu aliyefanyiwa vitendo vya ukatili,uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa unatajwa kuathirika kwa kupoteza nguvu kazi.
 
Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amesema serikali imekuwa ikiwekeza zaidi kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya elimu, Afya, barabara na reli na lengo ni jamii kutumia miundombinu hiyo kwa maslahi yao na Taifa hivyo ikiwa jamii moja inamaumivu yanayotokana na vitendo vya ukatili  inakuwa  vigumu kutumia vyema miundombinu hiyo na kujikuta Taifa linakuwa na jamii yenye vinyongo na  chuki.


 

Post a Comment

0 Comments