WAJAWAZITO WAASWA KUTOTUMIA DAWA ZA ASILI KUONGEZA UCHUNGU

 


Na Anthony Kayanda, Kigoma.

 Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuwa makini dhidi ya ongezeko la matumizi ya dawa asili zinazotumiwa na kinamama wajawazito kwa ajili ya kuongeza uchungu na kufungua njia ya uzazi kwa sababu zinasababisha vifo wakati wa kujifungua.

Mwito huo umetolewa na katibu wa Asasi ya kiraia ya Nguruka Development Agency (NDA), Dk. Staford Chamgeni ambapo imani potofu katika jamii ibadaiwa kuwa kiini cha baadhi ya kinamama kutumia dawa hizo.

"Hizi dawa za kiasili mara nyingi husababisha uchungu mkali na hata kupasua mfuko wa uzazi, wakati mwingine huweza kusababisha uambukizo mkubwa kwenye njia ya mfuko wa uzazi," amesema Dk. Chamgeni.

Ametaja mambo mengine yanayosababisha vifo vya mama na mtoto ni kuchelewa kuanza mahudhurio ya kliniki kwa vile inakuwa vigumu kwa wataalamu wa afya kuchelewa kujua dalili za hatari kwa mjamzito.

Mjamzito kushindwa kufanya maandalizi ya awali hususani namna ya kufika kituo cha huduma ya afya wakati anapopata uchungu au anapohisi tatizo la uzazi linaloweza kuhatarisha maisha yake.

"Changamoto nyingine ni kukosekana kwa wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa muhimu katika baadhi ya vituo vya huduma za afya kwa ajili ya kukabiliana na dharula yoyote ya uzazi inayoweza kutokea kwa mama na mtoto mchanga," amesema Dk. Chamgeni.

Asasi hiyo ya NDA yenye madaktari watatu wamejikita katika kutoa elimu ya afya ya uzazi katika vijiji vya wilaya ya Uvinza na wilaya nyingine mkoani Kigoma ili kupunguza vifo vya kinamama na watoto wachanga.

Baadhi ya watu wameridhishwa na huduma inayotolewa na Asasi hiyo kwani elimu wanayotoa inawafanya watu kuwa makini na kuzingatia vema kusaidi kinamama wajawazito. 

Mkazi wa Nguruka katika wilaya ya Uvinza, Hamisa Masudi amesema elimu wanayopewa imeongeza hamasa kwa kinamama kuhudhuria kliniki mapema na kuwahi vituo vya huduma kwa ajili ya kujifungua.

"Kinamama walikuwa na tabia ya kutumia madawa ya kienyeji (dawa za asili) kuongeza uchungu na kufungua njia ya uzazi lakini ni kweli baadhi walipata matatizo na kufariki wakati wa kujifungua," amesema Hamisa.

Mkazi wa Itebula wilayani Uvinza, Issa Genyeza amesema baada ya kupata elimu ya afya ya uzazi amekuwa makini kuhakikisha anamsindikiza mke wake kliniki kila anapotakiwa kuhudhuria.

Amesema huwa anamsindikiza mke wake kituo cha afya anapofikia muda wa kujifungua kwa sababu anatambua kuwa endapo itatokea uzazi pingamizi ni rahisi wataalamu wa afya kutoa msaada na hivyo kuokoa maisha ya mama na mtoto.

.

Post a Comment

0 Comments