Na Mwajabu Hoza, Kigoma.
WATAALAM
wa Afya mkoani Kigoma wameeleza kufanya
uhamasishaji katika jamii kuhusu zoezi la Utoaji wa Chanjo ya Polio kwa Watoto
walio na umri chini ya miaka 5 ili kuhakikisha huduma inatolewa kikamilifu kwa
lengo la kupambana na maambukizi ya Ugonjwa huo.
Zoezi hilo la chanjo ya Polio linatarajiwa kuanza
tarehe 28 ya April hadi Mei mosi ya mwaka huu ambapo takribani watoto 547,000
watafikiwa na huduma ya chanjo na watoto wengine Elfu 42 kutoka Kambi za
wakimbizi Za Nduta na Nyarugusu Mkoani Kigoma.
Akizungumza hatua hiyo ya utoaji wa chanjo kwa watoto
walio na umri chini ya miaka mitano Mganga mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt Jesca
Lebba amesema zoezi hilo linaendana sambamba na utoaji wa elimu juu ya umuhimu
wa chanjo kwa watoto hao ambapo elimu hiyo itahusisha zaidi wazazi na viongozi
ili kuhakikisha zoezi linafanikiwa.
Amesema
zoezi la chanjo limekuja katika jamii mara baada ya kutokea kwa mlipuko wa
ugonjwa huo katika eneo la Lilogwe nchini Malawi na kuna uwezekano mkubwa wa
kusambaa na kuadhiri maeneo mengine na hivyo serikali ikaona ipo sababu ya
kuanza kutoa chanjo hiyo kwa watoto.
“Ugonjwa huu ni virusi ambavyo huambukizwa kupitia kinyesi na
hauna tiba isipokuwa chanjo na unashambulia mishipa ya fahamu na unaweza
kusababisha mtoto kupooza na tiba yake pekee ni chanjo pekee ambayo haina
madhara yoyote kwa mtoto na tunaitoa chanjo hii kwa sasa kutokana na mlipuko
uliojitokeza" Amesema Jesca Lebba
Amesema maeneo ambayo yatatiliwa mkazo zaidi ni maeneo ya mipaka
ambayo yapo katika hatari kubwa ya maambukizi kutokana na jamii ya maeneo hayo
kuwa na muingiliano mkubwa wa watu ambao wanaingia na kutoka nchini.
Jesca amesema chanjo hiyo ni muhimu na itatolewa kwa njia
tofauti tofauti ikiwemo nyumba kwa nyumba , kwenye vituo vya kutolea huduma ,
pamoja na maeneo ya shuleni ambapo wahudumu wa afya watafika kwenye maeneo yote
muhimu ambayo watoto wanapatikana.
Kwa upande wa wadau wa afya wakiwemo shirika la Afya
Duniani WHO Dkt Gerald Marwa ameeleza ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa
na kufikia lengo lililokusudia na serikali ni lazima elimu itolewe ili kuondoa
imani potofu iliyopo ndani ya jamii kuhusu chanjo hiyo na sababu
zinazosababisha kutolewa kwa sasa.
Hata hivyo katika utekelezaji wa mpango Jumuishi wa
Taifa wa malezi, Makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto PJT-MMMAM wa Mwaka
2021/2022 hadi 2025/2026 serikali imeendelea kutoa huduma bora za afya
kwa maendeleo na ukuaji timilifu wa watoto kwenye masuala ya chanjo na dawa za
minyoo kwa lengo la kuwakinga watoto na maambukizi ya magonjwa
mbalimbali.
Imeelezwa
kuwa chanjo za watoto nchini Tanzania zimetolewa kwa zaidi ya asilimia 95 na
hilo linatokana na muamko wa jamii kutambua umuhimu wa watoto kupata chanjo
kupitia elimu inayotolewa na wataalamu wa afya.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengeye akatoa msisitizo
kwa watumishi wa serikali kutokuwa kikwazo katika utekelezaji wa zoezi hilo na
kuwataka watumishi wote kwa nafasi zao walizonazo kulisimamia vyema zoezi hilo
kwa maslahi ya watoto na taifa kwa ujumla.
“Watoto wetu hawawezi kuadhirika kwa hili , tunatakiwa
kuwa mstari wa mbele katika kampeni hii kuhakikisha tunawatetea na kuwakinga
watoto hawa ambao ni malaika wasio na uwezo wa kujitetea wao wenyewe hivyo ni
jukumu letu kuwatetea kwa kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo hii ili tuweze
kuwa na Taifa lenye nguvu hapo badae”
Baadhi
ya wananchi wametoa maoni yao juu ya chanjo hiyo ambapo wamesema kuna umuhimu
mkubwa kwa watoto kupatiwa chanjo ya Polio kwa kuwa wapo katika hatari kubwa ya
kupata maambukizi
"
Watoto wetu wadogo mara nyingi wanacheza hovyo maeneo mbalimbali na ugonjwa huu
unasambaa kupitia njia mbalimbali hivyo katika michezo yao anaweza kupata
maambukizi lakini kama atakuwa ameshapata chanjo itakuwa vigumu kwa mtoto
kupata adhari kupitia ugonjwa huu"
Aidha
walitoa ushauri kwa serikali kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo ikiwa ni
pamoja na kuwafikia wale waliopo majumbani kutokana na baadhi ya wazazi kuacha
kuwapeleka watoto wao cliniki kupata huduma mbalimbali ikiwemo chanjo.
0 Comments