SHIRIKA LA WORLD VISION LAZINDUA SHINDANO LA UANDISHI WA INSHA KWA SHULE ZA MSINGI

 


Diana Rubanguka,  Kigoma.

Shirika la World vision Tanzania (WVT) limezindua shindano la insha kwa shule za msingi katika maeneo ya mradi wanayosimamia ndani ya mikoa 12 kati ya 16 ikiwa ni sehemu ya kuwapa watoto nafasi ya kupaza sauti zao ikiwa ni njia mbadala za kuondokana na ndoa za utotoni na mimba za utotoni.

Hayo yameelezwa na  Kaimu Meneja wa shirika hilo Vincent Kasuga ambapo alisema, wanafunzi 100000 kuanzia darasa la tano hadi la saba wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo kuanzia ngazi ya shule, 5440 kutoka ngazi ya kata ndani ya shule 544 za msingi nchini.

Kagusa alisema kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye changamoto ya mimba na ndoa za utotoni ambapo kwa  kipindi cha 2020, wasichana watatu kati ya kumi huolewa kabla ya miaka 18.

Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma David Mwamalasi alisema, suala la kuacha shule kwa sababu tofauti ikiwemo mimba ni kubwa mkoani hapa  na kwa mwaka 2020-2021 wasichana 6123 walikatisha masomo kwa ngazi ya shule za msingi huku 200 ikiwa kwa sababu ya mimba na 676 kutoka sekondari.

"Wanafunzi 28 wa sekondari wameacha shule sababu ya ujauzito kwa mwaka 2022 kwa kipindi cha Januari hadi Februari" alieleza Mwamalasi

Katika mkutano wa elimu uliofanyika  Machi 7, 2022, walibaini kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia  changamoto hiyo ni ukosefu wa huduma ya chakula shuleni na hali hiyo  huchochea vitendo vya ngono

Mgeni rasmi katika gafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Easter  Mahawe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma alitoa wito kwa viongozi wa dini kufikisha elimu ya kupinga mimba za utotoni kwa kuwa wanayo mafasi ya kufikia jamii kwa urahisi kupitia waamini wao.

"Kwa sasa maadili yamepolomoka katika  jamii, binadamu wamekosa hofu ya Mungu  na kusababisha matokeo ya ukatili usioisha ndani ya jamii, tusaidiane kukomesha vitendo hivyo kwa kutoa elimu" Alisema mahawe.

Kwa upande wake kaimu katibu tawala MkoaMaxmillian Ngasa alisema jukumu la jamii nzima  kuwalinda watoto wetu dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa maslahi ya taifa letu.

Mmoja wa watoto kwa niaba ya wengine Subira Jonas kutoka shule ya msingi Nyakitonto alisema sababu kubwa ya mimba za utotoni na ndoa za utotoni ni wazazi kujitenga na watoto, na kutowapa elimu ya vitendo hivyo.

"Wazazi wengi hawana muda wa kuzungumza na watoto wao, na wakati mwingine wanakua bize na shughuli za mashambani" aliseleza subira

 

Post a Comment

0 Comments