WANANCHI WAJITOKEZE KUHESABIWA SIKU YA SENSA 2022 - MAKINDA.



Na Anthony Kayanda, Kigoma.

 Kamisaa wa sensa ya watu na makazi, Anna Makinda amewataka wananchi wajitokeze kuhesabiwa siku ya sensa ili serikali ipate takwimu sahihi ya idadi ya watu nchini.

Ametoa kauli hiyo jana wakati wa kikao cha makamisaa wa sensa kilichofanyika katika ukumbi wa RAS mjini Kigoma ambapo amesisitiza umuhimu wa kupata takwimu sahihi.

Amesema hadi sasa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 81 na takwimu zitakazokusanywa zitatumika kupanga mipango ya serikali kitaifa na kimataifa.

Kamisaa wa sensa kutoka Zanzibar, Balozi Mohamed Ally Hamza amesema sensa  ya mwaka huu 2022 itaendeshwa kwa mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Amesema kutakuwa na madodoso kuhusu taarifa za kaya juu ya idadi ya watu, huduma za jamii katika eneo husika, taarifa za majengo na anuani za makazi.

Amewataka watakaopata dhamana ya kusimamia zoezi la sensa mwaka huu kufanya kazi kwa uadilifu ili wasipotoshe takwimu.

Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amesema kamati za sensa zimeundwa kuanzia nazi ya mkoa, wilaya, kata, mitaa, vijiji na vitongoji.

Amesema mkoa wa Kigoma una kata 139, vijiji 306, mitaa 197, vitongoji 1838 na maeneo mengine ya kuhesabia watu yapo 2267.

Andengenye amewataka viongozi serikali, taasisi mbalimbali na jamii kwa jumla kuhakikisha kila mtu anakuwa balozi wa kuhamasisha watu ili washiriki sensa mwaka huu.

Uongozi wa mkoa umejipanga kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza wakati huu wa maandalizi ya sensa ya watu na makazi.

 


Post a Comment

0 Comments