WANAUME KUTOSHIRIKI UZAZI WA MPANGO KUNAONGEZA UMASIKINI KWENYE KAYA.

 


Na Anthony Kayanda, Kigoma.

Ushiriki duni wa wanaume katika elimu ya uzazi wa mpango ni mojawapo ya chanzo cha umasikini katika kaya nyingi, hususani kwa watu wanaoishi vijijini.

Hayo yameelezwa na mratibu wa asasi ya Tanzania Participatory & Rural Development Organization (TAPRUDO), Eunice Katabwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini kigoma.

Amesema wanaume wengi wamekuwa na mtazamo hasi wa kushiriki masuala ya uzazi wa mpango ambapo wanadhani jukumu hilo ni la wanawake pekee.

"Tumekutana na baadhi ya wanaume wakati wa kuelimisha jamii juu ya mambo mbalimbali na mtambuka lakini wengi wamekuwa wakisema mambo ya uzazi wa mpango ni ya wanawake, dhana hii ni mbaya na lazima wanaume waelimishwe kujua athari yake," alisema Eunice.

Amesema kutokana na wanaume hao kutojua faida ya kuzaa kwa mpango matokeo yake ni kuwasababishia madhara ya kiafya kinamama kwani wengi wamejikuta wakizaa maravkwa mara.

"Utamkuta mama mwaka huu anabeba mimba na mwakani mtoto, akinyonyesha mwaka mmoja mimba nyingine, sasa katika mazingira ya aina hii unategemea huyu mama atapata muda wa kuzalisha mali na ukizingatia wengi ni wakulima huko vijijini? amehoji Eunice.

Ili kuleta maendeleo katika jamii lazima familia nzima washirikiane katika kazi ya uzalishaji mali, hivyo lazima mama awe na nguvu ili azalishe kikamilifu.

Ametoa mwito kwa taasisi na mashirika mbalimbali kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wanaume kwani wakifahamu vizuri itasaidia kupanga uzazi na hivyo afya ya wanawake itaimarika.

Baadhi ya watu waliotoa maoni kuhusu wanaume kupata mafunzo ya uzazi wa mpango wamesema jambo hilo ni muhimu kwa vile litapunguza migogoro katika familia na litaongeza ushirikiano katika uzalishaji mali.

Mkazi wa kijiji cha Msimba, Awamu Hussein amesema wanaume wengi hawana utaratibu wa kuwasindikiza wake zao kliniki, hivyo elimu ya uzazi inayotolewa na wauguzi inaishia kwa wanawake tu.

"Ikiwa na sisi wanaume tutakwenda kliniki na wake zetu itasaidia kujua changamoto zinazowakabili wanawake kuanzia wakati wa mimba, kujifungua hadi kunyonyesha," amesema Hussein.

Amesema kuzaa mfululizo na mara kwa mara kunamfanya mwanamke achoke na kupoteza uwezo wa kufanya kazi hususani kilimo ambayo ndio uti wa mgongo kwa wakazi wengi wa vijijini.

Kuruthumu Maulidi wa Katubuka mjini Kigoma amesema wanaume wengi wanaona haya kufuatana na wenza wao kliniki kwa madai kwamba mambo ya kliniki hayawahusu.

Amesema wengi wanalazimika kwenda na wenza wao siku ya kwanza mama anapoanza kliniki kwa sababu ni lazima apimwe vipimo vingi vya afya ambayo ni lazima pia mwanaume ahusishwe.

"Baada ya hapo humuoni tena mwanaume kwenda kliniki lakini (wanawake) tumezoea na tunaona ni suala la kawaida tu," alisema.

John Daudi wa Majengo mjini Kigoma amesema itakuwa jambo gumu kwa wanaume kushiriki mambo ya uzazi kwa sababu elimu hiyo inatolewa zaidi kliniki.

Ametaka serikali iweke utaratibu wa kutoa elimu ya uzazi wa mpango hadi mahali pa kazi ili iwe rahisi wanaume wengi kufikiwa badala ya kutegemea waende kliniki na wake zao.

Mkoa wa kigoma ni mojawapo ya mikoa inayoendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi na uzazi salama kwa jamii kupitia serikali na mashirika binafsi na asasi za kiraia.

 

Post a Comment

0 Comments