JAMII YAELIMISHWA JUU YA DALILI MBAYA KWA WAJAWAZITO

Na Anthony Kayanda, Kigoma.

Ili kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua, jamii mkoani Kigoma imetakiwa kujua dalili za hatari kwa mama anapokuwa mjamzito.

Akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kata ya Nguruka katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, katibu wa asasi ya Nguruka Development Agency (NDA), Dr. Staford Chamgeni alisema vifo vingi vinatokana na jamii kushindwa kuelewa dalili za hatari kwa mama mjamzito.

Alitaja viashiria vya hatari kwa mama mjamzito kuwa ni pamoja na kutoka damu, kuvimba miguu, kifafa cha mimba na maambukizo katika mfuko wa uzazi.

"Viashiria hivi vya hatari visipodhibitiwa mapema na wataalamu wa afya vinaweza kusababisha mama mjamzito kupoteza maisha, mimba kuharibika au mtoto kufariki pindi tu anapozaliwa," alisema Dr. Chamgeni.

Ili kuepuka hatari hizo, jamii imetakiwa kuhakikisha mama mjamzito anapata lishe bora, anatumia chandarua chenye dawa, anatumia dawa za katibu minyoo na kuhakikisha damu yake inakuwa ya kutosha.

"Kila mmoja anatakiwa kuhakikisha mama mjamzito anajifungulia katika vituo vya huduma za afya kwa sababu endapo itatokea changamoto yoyote wakati wa kujifungua ni rahisi kupata huduma inayostahili na ikishindikana atapewa rufaa kwenda hospitali kubwa," alisema Dr. Chamgeni.

Dr. Chamgeni alitaja mambo yanayochangia vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ni pamoja na mama kuchelewa kuanza kliniki, jambo ambao linasababisha viashiria vya hatari visionekane mapema.

Wanaume kutohudhuria kliniki husababisha kushindwa kutoa msaada wa haraka kwa wajawazito kwa kuwa wanakuwa hawajui namna ya kutoa msaada.

Nyingine ni mama mjamzito kukosa maandalizi ya awali kama vile ni kwa njia gani atafika kituo cha huduma za afya wakati wa kujifungua, kukosa mtu wa uhakika anayetakiwa kumwambia pale inapotokea tatizo la uzazi linaloweza kuhatarisha maisha yake.

Kufuatia mafunzo hayo, baadhi ya watu walishukuru asasi ya NDA kwa kuwajengea uwezo juu ya masuala ya afya ya uzazi.

Mkazi wa Nguruka, Jason Emanuel alisema watu wengi wamenufaika na elimu ya afya ya uzazi inayotolewa na asasi ya NDA kwani wamepata ujuzi utakaowasaidia kutoa huduma kwa kinamama wajawazito.

Alisema wakazi wa Nguruka wataweza kusaidiana na wataalamu wa afya kupunguza vifo vinavyoweza kutokea kwa sababu wataweza kutoa huduma ya kwanza kwa wajawazito na hivyo kuepusha hatari ya kutokea vifo visivyo na lazima.

Rehema Omary wa Itebula alisema kutokana na elimu wanayopewa itasaidia kuokoa maisha ya mama wajawazito na watoto wachanga kwa sababu wanajua viashiria vya hatari na namna ya kutatua changamoto hizo.

 

Post a Comment

0 Comments