HALMASHAURI ZITUNGE SHERIA KUWABANA WANAUME WASIOHUDHURIA KLINIKI

 


Na Anthony Kayanda, Kigoma.

 Mara kadhaa imekuwa vigumu kuwashawishi wanaume kuhudhuria Kliniki wakiambatana na wenza wao wakati wa ujauzito, na jambo hili linaonekana kukwama.

Kuna wakati Wizara ya Afya iliamua kwamba mama mjamzito hatapata huduma kama hakwenda na mwenza wake anapohudhuria Kliniki kwa mara ya kwanza pindi anapopata ujauzito.

Sharti hili lilisababisha wanaume kufika Kliniki wakiambatana na wenza wao, wakaelimishwa juu ya mambo muhimu ya kufuata kipindi hicho cha ujauzito na kupimwa vipimo mbalimbali ili kujua kama wameambukizwa magonjwa ya zinaa, virusi vya ukimwi au maradhi mengine.

Bado kuna changamoto kwa baadhi ya kinamama wajawazito kushindwa kufika Kliniki au kutohudhuria kwa wakati ambapo muda sahihi wa kuanza Kliniki ni chini ya wiki 12 baada ya kupata mimba, lakini ni wachache.

Wakati wa hotuba ya Wizara ya Afya kwenye Bunge la bajeti mwaka huu kuhusu makadirio ya mapato na matumizi, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa takwimu mbalimbali kuhusiana na afya ya uzazi na uzazi wa mpango.

Alisema ili kuhakikisha watu wanatumia njia za uzazi wa mpango, serikali kupitia Bohari ya dawa nchini (MSD) ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango dozi 1,755,359 sawa na asilimia 82 ya lengo.

Sindano za uzazi wa mpango aina ya Depo - Provera zilikuwa dozi 2,125,625 sawa na asilimia 93 ya lengo, vipandikizi 206,000 sawa na asilimia 78 ya lengo. Dawa hizo zilisambazwa Halmashauri zote nchini.

Waziri Ummy aliliambia Bunge kwamba wateja waliotumia njia za uzazi wa mpango kati ya Julai 2021 hadi Machi 2022 walikuwa 4,189,787 ikilinganishwa na wateja 4,357,151 mwaka 2020.

Waliotumia vipandikizi ni asilimia 57.1, sindano ni asilimia 18.5, vidonge walikuwa asilimia 10.1, watumiaji wa mipira ya kiume (kondomu) walikuwa asilimia 5.3 na kufunga kizazi kwa wanawake ni asilimia 0.4

Nyingine ni watumiaji wa njia ya kitanzi ambao walikuwa asilimia 7.2 na njia nyingine walikuwa asilimia 1.4 ambapo takwimu hizi ni kuanza Julai 2021 hadi Machi 2022.

Kwa kawaida wengi wa watumiaji wa njia hizi ni wanawake kwa sababu mbalimbali hususani za kibaiolojia. Mwitikio wa wanaume katika kutumia njia za uzazi wa mpango bado upo chini.

Wanaume ni sehemu ya jamii na wanao wajibu mkubwa kuhakikisha masuala yanayohusu uzazi wa mpango yanapewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo kwenye Kaya na serikali.

Ili mipango ya maendeleo ifanyike kikamilifu ni lazima wanaume wawe na uelewa wa kutosha juu ya uzazi wa mpango, vinginevyo jukumu hilo litabaki kwa wanawake peke yao.

Mratibu wa Asasi ya kiraia ya Tanzania Participatory and Rural Development Organisation (TAPRUDO), Eunice Katabwa alisema jamii ingekuwa na uelewa unaofanana kuhusu uzazi wa mpango, jamii ingenufaika vya kutosha.

"Mara nyingi ukienda Kliniki utawakuta wanawake ndio wengi, ikitokea umeona mwanaume basi atakuwa mmoja au wawili, na huyo baadhi ya watu watakuwa wanamshangaa," alisema Eunice.

Asasi ya TAPRUDO imejikita katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ikihamasisha jamii kufanya shughuli za maendeleo hasa kilimo ili wapate kipato kusaidia kaya.

Ili kuhakikisha wanaume wanahudhuria Kliniki kupata elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango inayotolewa na wataalamu wa afya ni lazima wafike Kliniki kujifunza kama ilivyo kwa wanawake.

Jambo la muhimu ni kwa Halmashauri zote nchini kuanza kutunga sheria ndogondogo (by laws) kwa ajili ya kuwabana wanaume wanaokwepa kuhudhuria Kliniki wakiambatana na wenza wao.

Diwani wa Kata ya Mungonya katika Halmashauri ya wilaya Kigoma, Abasi Dunia alisema itakuwa vema kama wanaume wengi watapata elimu ya uzazi wa mpango kwani itasaidia kurahisisha upangaji wa mipango ya maendeleo katika Halmashauri kwa urahisi.

"Baadhi ya familia zimeingia katika migogoro kwa sababu ya ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya uzazi wa mpango, utakuta mama anabeba ujauzito halafu baba anakasirika kwa sababu hawakupanga mama abebe ujauzito," alisema Abasi.

Aliongeza kwamba "kama familia ingekuwa na uelewa wa pamoja juu ya matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango na namna bora ya kuamua mama ashike mimba wakati gani, kusingekuwa na migogoro ya aina hiyo."

Njia mojawapo ya kusaidia jamii kwa kuwafanya wanaume kuhudhuria Kliniki ili wawe na uelewa mzuri wa masuala ya uzazi wa mpango kama wanawake ni kuzishawishi mamlaka za serikali za mitaa au serikali kuu kutunga sheria itakayowabana wanaume wanaokataa kuhudhuria Kliniki.

 

 

Post a Comment

0 Comments