Na
Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa dini hawana budi kuendelea kuiombea
amani Tanzania pamoja na viongozi wake kwani bila amani hata kusanyiko la
kidini haliwezi kufanyika.
Akinukuu
Quran tukufu sura ya 2, aya ya 126 (Quran 2:126), Waziri Mkuu amesema nabii
Ibrahim aliuombea mji wake na wakazi wake amani na neema kutoka kwa
Mwenyezi Mungu.
“Nami
nitoe rai kwa viongozi wetu wa dini, waendelea kuiombea nchi yetu na viongozi
wake ili waendelee kuliongoza vema Taifa letu ikiwa ni pamoja na kujenga umoja
na mshikamano, kudumisha amani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”
Ametoa
wito huo leo (Jumapili, Agosti 14, 2022) kabla ya kukabidhi tuzo kwa mshindi wa
kwanza wa kuhifadhi Quran barani Afrika katika mashindano yaliyofanyika kwenye msikiti
wa Mfalme Mohammed VI, ulioko Kinondoni makao makuu ya BAKWATA, jijini Dar es
Salaam. Mashindano hayo yamefadhiliwa na Taasisi ya Mfalme wa Morocco Ulamaa
Afrika.
Akizungumza
kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema kusanyiko
hilo ni kielelezo cha utukufu wa Quran barani Afrika kwani limejumuisha
washiriki 88 kutoka nchi 34 barani Afrika.
Amesema
katika zama hizi dunia inashuhudia kuongezeka kwa vitendo viovu ikiwemo watoto
kuuwa wazazi wao; ulawiti; ubakaji hususani kwa watoto na wanafunzi; watoto na
vijana kutowaheshimu watu wazima; uvaaji wa mavazi yasiyo na stara hususani kwa
wasichana na wavulana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Amesema
Quran inapaswa kuwa chanzo cha kutegemewa cha mafunzo sahihi ya tabia njema,
utii na kuheshimu mamlaka zilizopo. “Tukiwalea vijana wetu katika mafunzo haya
tutakuwa tunamsaidia mlezi wetu namba moja Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan
ambaye anaguswa na suala zima la maadili hususan kwa vijana kuwa na wasaidizi
wacha Mungu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao.”
Waziri
Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini wahakikishe kuwa vijana wanaweza kuhifadhi
Quran lakini pia wawe wamehitimu katika fani mbalimbali. “Kijana akihitimu fani
yake siyo rahisi kumuona akienda kinyume na maadili ya taaluma yake. Kwa hiyo,
Quran ni mchunga wa nafsi ya mtaalamu huyo na hivyo, kumfanya aonyeke
dhidi ya kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na uadilifu.“
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo ya kutoa tuzo kwa washindi,
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir alimshukuru Mfalme wa VI wa
Morocco na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mfalme wa Morocco Ulamaa Afrika, Bw.
Mohammed Rifqiy kwa kuamua kuleta mashindano hayo Afrika Mashariki.
“Uamuzi
wao wa kuleta mashindano haya umetuwezesha kuona jinsi Quran ilivyokuwa
inaandikwa kwa mkono hadi kufikia hatua ya sasa ya kuchapisha. Wenzetu wa
Afrika Magharibi wamezoea kuyaona haya.”
Miongoni
mwa washindi waliotia fora ni binti wa miaka 14, Saima Hassan Suleiman wa Dar
es Salaam ambaye aliibuka mshindi wa kwanza katika kundi la pili la kusoma
Quran na kuhifadhi juzuu 30.
Saima
ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Shaaban
Robert ya jijini Dar es Salaam, alisema amekuwa akijifunza Quran tangu
alipokuwa na miaka mitano. Kundi hilo lilikuwa na washindi wawili wa Tanzania
akiwemo Ahmed Salum Mbweta ambaye ameibuka mshindi wa tatu.
Mshindi
wa kwanza katika kundi la kwanza la kusoma na kuhifadhi Quran kwa mtindo wa
riwaya ya warshi (Riwayat Warsh) ni Murtado Olatunji Katibi wa Nigeria. Wa pili
ni Abdinassir Hassan Ibrahim kutoka Somalia na wa tatu ni Khatry Dakhay kutoka
Mauritania.
Katika
kundi la tatu ambalo ni la tajwid, mshindi wa kwanza alikuwa ni
Ustaadh Ahmad Salim Mbwewa ambaye ni mwalimu wa watoto jijini Dar es Salaam.
0 Comments