Na Mwajabu Hoza,
Kigoma.
MKOA wa Kigoma umetoa chanjo ya Polio 642,714
kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ikiwa ni sawa na asilimia 107 na lengo
likiwa ni kupambana na virusi vya ugonjwa huo kwa watoto.
Akizungumzia hilo Mganga mkuu wa mkoa wa
Kigoma Jesca Lebba amesema makisio ya mkoa ilikuwa ni kutoa chanjo kwa watoto
593, 277 ambapo hadi kukamilika kwa zoezi la utoaji wa chanjo ya Polio kulikuwa
na ongezeko la watoto 49,437 waliopata chanjo hiyo.
Amesema mkoa ulitenga vituo maalumu vya
kutolea chanjo pamoja na maeneo ya kutolea huduma za afya ambapo jumla ya vituo
256 vilitumika kutoa chanjo hiyo kwa watoto, maeneo ambayo jamii iliweza kufika
kwa urahisi zaidi.
Dtk Lebba amesema katika utekelezaji wa zoezi
la utoaji wa chanjo kwa watoto serikali ya mkoa wa Kigoma ilipokea zaidi ya
shilingi milioni 70.5 kupitia ufadhili wa UNICEF huku wadau wengine wakiwa ni
WHO.
Amesema mafanikio yaliyojitokeza yametokana
na ushirikiano wa wadau wengine wakiwemo waandishi wa Habari ,
mashirika mbalimbali ikiwemo IRC ,CRS, THPS , MTI, RED CROSS, PATHIFINDER.
Akielezea chanzo cha kutoa chanjo hiyo kwa
watoto chini ya umri wa miaka mitano amesema ni kutokana na taarifa za kuwepo
kwa mlipuko wa ugonjwa wa polio katika eneo la Lilongwe nchini Malawi
ambapo amesema ugonjwa huo husambaa kwa kasi na kuadhiri zaidi watoto
wadogo.
“Ugonjwa huu unatokana na virusi na
hauna tiba isipokuwa chanjo pekee na huambukizwa kupitia kinyesi na kushambulia
mishipa ya fahamu na kusababisha mtoto kupooza”
Hatua hivyo ya utoaji wa chanjo mbalimbali
kwa watoto nchini Tanzania jamii imeelezwa kuwa na muamko mkubwa kwa asilimia
95 na hilo linatokana utekelezaji wa sera pamoja na mpango Jumuishi wa
Taifa wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto PJT-MMMAM ambao umekuwa
ukizungumziwa sana na serikali katika kuelimisha jamii.
Ukiachilia mbali mafanikioa hayo lakini
pia Dkt. Lebba ameeleza baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa
utekelezaji wa zoezi hilo kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, miundombinu kwa
baadhi ya maeneo ni changamoto kuifikia kwa urahisi.
Baadhi ya wananchi akiwemo Joseph Kalyongwa
ameeleza kutokana na elimu pamoja na hamasa inayotolewa na wataalamu wa afya
kuhusu chanjo mbalimbali imesaidia jamii kuwa na uelewa wa kujitokeza kwa wingi
kupata chanjo ili kulinda afya zao.
"Tuna imani kubwa na wataalamu wa afya
kutika kulinda afya kinachohitajika ni elimu iendelee kuwafikia wananchi
hususani wale waliopo vijijini hususani maeneo ambayo hayafikiki kiurahisi
miundombinu yake bado si mizuri" alisema
Kampeni ya chanjo hiyo ya Polio ilitekelezwa
mkoani Kigoma kwa kipindi cha siku nne kuanzia Mei 12 hadi 15 ya mwaka
2022.
0 Comments